Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mnigeria Tijjan Muhammad-Bande ateuliwa kuongoza mkutano wa 74 wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa

Balozi Tijjani Mohammad-Bande, Rais mteule wa mkutano wa 74 wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa (4 Juni 2019)
UN / Evan Schneider
Balozi Tijjani Mohammad-Bande, Rais mteule wa mkutano wa 74 wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa (4 Juni 2019)

Mnigeria Tijjan Muhammad-Bande ateuliwa kuongoza mkutano wa 74 wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa

Masuala ya UM

Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, leo limemchagua mwanadiplomasia na mwanazuoni kutoka Nigeria Tijjani Mohammad Bande kuwa rais wa mkutano wa 74 wa baraza hilo utakaoanza mwezi Septemba mwaka  huu hadi Septemba mwakani.

Ni ndani ya ukumbi wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa kwenye makao makuu ya chombo hicho jijini New York Marekani, rais wa mkutano wa sasa wa 73 wa baraza hilo Maria Fernanda Espinosa akitangaza kwamba kwa mujibu wa vipengele vya ibara ya 60 ya uamuzi wa Baraza Kuu namba 34.401, namtangaza Mheshimiwa Tijjan Muhammad- Bande wa Nigeria kuwa amechaguliwa kwa kauli moja kuwa Rais wa mkutano wa 74 wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa.

Kisha Profesa Muhammad-Bande akiwa amevalia vazi la kitaifa la Nigeria akajongea kwenye jukwaa akiongozwa na afisa wa itifaki tayari kuelezea sera na vipaumbele vyake akisema kwamba, “utekelezaji wa majukumu ya sasa na ajenda 2030, nikipatia msisitizo amani na usalama, kutokomeza umaskini, njaa, kuboresha elimu, hatua dhidi ya mabadiliko ya tabianchi na ujumuishaji makundi yote, itakuwa vipaumbele vikuu vya mhula wangu wa urais.”

Rais huyu mteule wa mkutano wa 74 wa Baraza Kuu akazungumzia pia mizozo na usawa wa jinsia na kwamba “kwa kuwa Umoja wa Mataifa bado haujakidhi matakwa ya waasisi wetu, kwenye suala la kuzuia vita na mauaji, tunachukua wajibu wa pamoja wa kufanya dunia kuwa pahala bora, salama na penye amani. Kusongesha haki za binadamu na kuwezesha wanawake, vijana kunahitaji mtazamo wa kipekee, na nitapatia umuhimu usawa wa jinsia katika mfumo mzima wa Umoja wa Mataifa kuanzia kwenye ofisi yangu.”

Ukumbi wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa
UN /Manuel Elias
Ukumbi wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres akatumia hotuba yake kumpongeza Profesa Muhammad-Bande akisema kuwa ana imani ataleta  uzoefu wake tangu akiwa mwakilishi wa kudumu wa Nigeria kwenye Umoja wa Mataifa,  halikadhalika  uanazuoni na utaalamu wake kwenye masuala ya sayansi ya siasa na uongozi wa umma na zaidi ya yote, “ukiwa ni raia wa Nigeria na pia muafrika, una mtazamo muhimu sana kuhusu changamoto zinazokabili bara hilo kama vile kule  ukanda wa Sahel na bonde la Ziwa Chad na zaidi ya yote una mtazamo mpana juu ya changamoto zinazokabili dunia nzima kwenye misingi yetu mitatu ambayo ni amani, maendeleo endelevu na haki za binadamu.”

Kabla ya kuwa mwakilishi wa kudumu wa Nigeria kwenye Umoja wa Mataifa, Profesa Muhammad-Bande amewahi kuwa Makamu wa Rais wa mkutano wa 71 wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa na ameshiriki pia kwenye vikao  muhimu ikiwemo mwenyekiti wa kamati maalum ya Umoja wa Mataifa kuhusu ulinzi wa amani.

Halikadhalika amekuwa mjumbe wa Bodi shauri ya Umoja wa Mataifa kwa ofisi ya kukabili ugaidi na mwenyekiti wa kundi la jumuiya ya uchumi ya nchi za Afrika Magharibi, ECOWAS kwenye Umoja wa Mataifa kwa mwaka 2018-2019.