Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

FAO na wadau waungana kusimamia suala la ardhi za jamii Kenya

Ismail Isack Amin, mkulima mwenye umri wa miaka 66 ambaye anasema amekuwa akijinufaisha na ardhi  yenye rutuba nchini mwake Somalia tangu akiwa na umri wa miaka
UNSOM video screen capture
Ismail Isack Amin, mkulima mwenye umri wa miaka 66 ambaye anasema amekuwa akijinufaisha na ardhi yenye rutuba nchini mwake Somalia tangu akiwa na umri wa miaka

FAO na wadau waungana kusimamia suala la ardhi za jamii Kenya

Ukuaji wa Kiuchumi

Shirika la chakula na kilimo duniani, FAO nchini Kenya limeshirikiana na serikali na Muungano wa Ulaya ili kuimarisha uhakika wa chakula na lishe kupitia mbinu sawa na salama na usimamizi wa ardhi kwa ajili ya maisha bora na maendeleo ya kiuchumi na kijamii. 

Mradi huo ambao unaunga mkono dira ya serikali ya Kenya mwaka 2030 kupitia ugatuzi wa usimamizi wa ardhi ya jamii unanufaisha wakazi katika kaunti za Tana River, Turkana, Pokot magharibi, Baringo, Marsabit, Samburu, Laikipia na Nandi. 

Gabriel Rugalema ni mwakilishi mkazi wa FAO Kenya

(Sauti ya Rugalema)

“Kwa sababu ardhi ni muhimu sana kwa Kenya, ufikiaji wake na usimamizi wake ni muhimu ili Kenya iwe na mfumo wa usimamizi wake kwa ajili ya kuleta faida nyingi kutokana na uzoefu wa FAO kutoka nchi zingine kwa ajili ya kusaida usimamizi wa ardhi nchini humo.”

FAO imejikita katika mradi wa usimamizi wa ardhi za jamii kwa ajili ya kuhakikisha kwamba ardhi hizo zimesajiliwa, zinatambulika na zimegawanywa na kwamba wenyeji wanahusishwa katika ugawaji na usimamizi wa ardhi kwa ajili ya kuzuia matumizi mabaya na mizozo. 

Richard Chebon ni mwenyekiti wa chama cha wamiliki wa ardhi jamii ya Sabor

(Sauti ya Richard)

"Wanatupatia mafunzo kuhusu sheria mpya za ardhi, sisi wengine hatujasomea maswala ya Katiba lakini kupitia kwa FAO tumepata kujua kwamba mambo  yamebadilika kutoka umiliki wa kundi hadi umiliki wa kijamii."

Tayari mradi umeanza kuzaa matunda kama anavyoelezea Shelekudere kutoka jamii ya Sere Olipi

(Sauti ya Sherelekudere)

"Tangu kupokea mafunzo kutoka FAO, wanawake wameanza kujumuishwa kwenye kamati ya ardhi, nawapa changamoto kwamba iwapo kuna uchaguzi unafanyika, wajitokeze na kuwania viti vya ngazi ya juu ikiwemo mwenyekiti."