Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Usafiri wa baiskeli una faida za kiafya isitoshe kimazingira

Mradi wa baiskeli moja, msichana mmoja unaoendeshwa na shirika la kirai kwa ajili ya usafiri wa wanafunzi wasichana kuelekea na kutoka shuleni.
Msichana Initiative
Mradi wa baiskeli moja, msichana mmoja unaoendeshwa na shirika la kirai kwa ajili ya usafiri wa wanafunzi wasichana kuelekea na kutoka shuleni.

Usafiri wa baiskeli una faida za kiafya isitoshe kimazingira

Afya

Mahitaji ya wasafiri ambao hutembea kwa miguu au kuendesha baiskeli, ambayo ni idadi kubwa ya watu yanapuuzwa na mataifa mengi licha ya kwamba faida za kuwekeza katika usafiri wa kundi hili zinaweza kuokoa maisha, kusaidia kulinda mazingira na kupunguza umaskini.

Kauli hiyo ni kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa katika ujumbe wake wa kuadhimisha siku ya baiskeli duniani ambayo kila mwaka huadhimishwa Juni 3.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa leo kwa ajili ya siku hii kushughulikia mahitaji ya waendesha basikeli na wanao tembea kwa miguu ni  muhimu katika suluhu za usafiri na kusaidia miji kuimarisha hali ya hewa na usalama barabarani.

Shirika la afya ulimwenguni, WHO limesema mazingira salama ya kutembea na kuendesha baiskeli ni suala muhimu katika kufikia usawa wa kiafya kwani kwa watu maskini ambao hawana magari, kutembea na kuendesha baiskeli kunawapa mfumo wa usafiri ambao unapunguza hatari za kupata magonjwa ya moyo, baadhi ya saratani, kisukari na hata kufariki dunia na hivyo sio tu kuna faida za kiafya lakini pia gharama zake ni nafuu na rafiki.

Mbali na gharama zake, matumizi ya baiskeli ni safi na yanajali mazingira na kwa hiyo ni usafiri endelevu. Aidha baiskeli inaweza kutumika kwa ajili ya kuimarisha elimu, afya na michezo. Pia matumizi ya baiskeli yanachagiza ujumbe chanya kwa ajili ya matumizi endelevu na uzalishaji ambao hauna athari mbaya zinazochangia  mabadiliko ya tabianchi.