Madai 37 ya ukatili na  unyanyasaji wa kingono dhidi ya UN yawasilishwa robo ya kwanza ya mwaka huu pekee

30 Mei 2019

Ripoti mpya kuhusu ukatili na unyanyasaji wa kingono kwenye Umoja wa Mataifa imetolewa hii leo ikionyesha kuwa chombo hicho katika robo ya  kwanza ya mwezi huu kimepokea madai 37 ya vitendo hivyo.

Naibu Msemaji wa  Umoja wa Mataifa Farhan Haq akizungumza na waandishi wa habari mjini New  York, Marekani hii leo amesema madai hayo ya ukatili na unyanyasaji wa kingono ni dhidi ya wafanyakazi wa umoja huo wakiwemo raia, walinda amani, watendaji wa mashirika na miradi ya Umoja wa Mataifa.

Hata hivyo amesema hadi sasa si madai yote hayo yamethibishwa na kwamba idadi kubwa yapo katika hatua za awali za uchunguzi.

“Katika madai hayo 37 ya ukatili wa kingono na  unyanyasaji dhidi ya watendaji wa Umoja wa Mataifa, kuna manusura 49 ambapo 28 ni wanawake, 11 ni wasichana, 1 ni mvulana, 7 ni wanawake ambao umri wao haufahamiki, 1 ni mtu mzima umri haufahamiki na 1 ni mtoto ambaya hajafahamika,” amesema Bwana Haq.

Amechambua zaidi akisema katika visa hivyo 37, 16 ni ukatili wa kingono, 27 unyanyasaji wa kingono, visa vinne bado havijaweza kubainishwa ilihali 2 vimeelezwa kuwa ni matukio mengineyo na kisa kimoja hakijabainishwa.

Tayari kisa kimoja kimewasilishwa kwa nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa.

Naibu Msemaji huyo wa Umoja wa Mataifa amezungumzia pia madai mengine 33 ambayo Umoja wa Mataifa umepokea akisema kuwa yanahusisha watendaji ambao si wafanyakazi wa Umoja wa Mataifa bali ni wadau.

Wakati ripoti hii imetolewa, imeelezwa kuwa Umoja wa Mataifa unaendelea na juhudi za kutekeleza mkakati wa Katibu Mkuu wa kutokomeza ukatili na  unyanyasaji wa kingono ikirejelewa  ripoti yake aliyozindua mwaka jana kuhusu kutokomeza vitend hivyo ikiwemo kupatia kipaumbele haki na utu wa manusura, kuondokana na ukwepaji sheria na kushirikisha nchi wanachama na mashirika ya kiraia sambamba na kuweka uwazi katika kutokomeza vitendo hivyo.

Bwana Haq amesema pamoja na hatua hizo, Umoja wa Mataifa unaendelea kushawishi nchi wanachama zijiunge na mpango wa Katibu Mkuu wa kutokomeza ukatili wa kingono kwenye mizozo ambapo hadi sasa wanachama ni 74.

Halikadhalika Umoja wa Mataifa unasihi nchi wanachama kutia saini mkataba wa hiari  na Katibu Mkuu wa UN wenye ahadi ya kutokomeza ukatili wa kingono na unyanyasaji ambapo hadi sasa ni nchi 101 tu zimetia saini.

 

 

 

♦ Tafadhali iwapo unataka kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud