Ushindi wa tuzo ya Charlemangne ni heshima kubwa kwangu na UN- Guterres

Katibu Mkuu Antonio Guterres akipokea tuzo ya Charlemagne mjini  Aachen, Ujerumani tarehe 30/5/19
UNFCCC/James Dowson
Katibu Mkuu Antonio Guterres akipokea tuzo ya Charlemagne mjini Aachen, Ujerumani tarehe 30/5/19

Ushindi wa tuzo ya Charlemangne ni heshima kubwa kwangu na UN- Guterres

Masuala ya UM

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres hii leo amepokea tuzo ya Charlemangne huko mjini Aachen nchini Ujerumani na kusema kuwa ni heshima kubwa sana kwake.

Tuzo hiyo ambayo hutolewa kila mwaka tangu mwaka 1950, ni kwa ajili ya watu ambao wanaonekana wako mstari wa mbele kufanikisha muungano wa bara la Ulaya ambapo Guterres katika hotuba yake ya kupokea tuzo hiyo amesema, “ninatambua kuwa mnanituza kupitia mimi kutokana na ahadi, huduma na kujitolea kunakofanywa na wanawake na wanaume walioko Umoja wa Mataifa.”

Amesema kwa kufanya hivyo pia wanatia moyo uimarishaji wa ushirikiano kati ya kile ambacho amesema ni “miradi miwili mikubwa ya zama za sasa ambayo ni Umoja wa Mataifa na Muungano wa Ulaya,” na kwamba kitendo cha kumpatia tuzo kinaonyesha jinsi ambavyo wameona mbali.

Katibu Mkuu amesema ni kwa kuzingatia kuwa dunia ya sasa iko kwenye njia panda na ndio maana kupatiwa kwake tuzo hiyo kunamfanya awe mnyenyekevu zaidi akiwa na matumaini kuwa vyombo hivyo viwili; Umoja wa Mataifa na Muugano wa Ulaya vinaweza kuwa na matunda ya kipekee ya kunufaisha wakazi wa dunia katika zama za sasa zenye changamoto za mabadiliko ya tabianchi, uhamiaji na maendeleo ya teknolojia.

Amepigia chepuo umuhimu wa ushirikiano wa kimataifa akisema, “iwapo unataka kuepusha vita mpya baridi, iwapo unataka kuepusha mvutano baina ya pande mbili, pengine tofauti na ilivyokuwa awali, iwapo unataka kujenga ushirikiano wa kimataifa wa dhati, bila shaka tunahitaji Ulaya iliyoungana na thabiti kama ndio msingi wa nguzo ya ushirikiano wa kimataifa unaozingatia kanuni.”

 Bwana Guterres amesema kushindwa kwa Ulaya bila shaka kutadhoofisha na kutwamisha ushirikiano wa kimataifa duniani akienda mbali akieleza kuwa Umoja wa Mataifa unahitaji Ulaya iliyo thabiti na iliyoungana.

Hata hivyo amesema ili hilo liwezekane, bara la Ulaya linapaswa kutambua baadhi ya changamoto kubwa ambazo inalikabili akisema kuwa, “ nafikiri kile kinachodhoofisha bara hili ni suala la wakazi wenyewe kutomiliki masuala  yanayohusu bara la Ulaya.”

 Hata hivyo amesema ameanza kuona dalili ya mabadiliko ya mwenendo huo hivi karibuni kwa kuanzia na ongezeko la idadi ya wapiga kura kwenye chaguzi za Ulaya.

Mwezi Januari mwaka huu Guterres alitangazwa mshindi wa tuzo hiyo ambapo bodi husika ilisema sababu kubwa ya ushindi wake ni jinsi alivyojitolea kuchechemua na kusongesha ushirikiano wa kimataifa kwa misingi ya maadili na malengo ya Muungano wa Ulaya na Umoja wa Mataifa.

Bodi hiyo ilisema kuwa ni katika zama ambazo misingi  ya kidemokrasia nay a kibinadamu  inakumbwa na tafrani, Guterres amekuwa mtetezi wa kipekee wa muundo wa jamii ya Ulaya, akitetea stahmala, mazungumzo na jamii zinazopokea wageni.