Genge la watu kumbaka mtoto wa miaka 9 ni unyama usiostahili:UNFPA

30 Mei 2019

Shirika la Umoja wa Mataifa la idadi ya watu duniani UNFPA leo limelaani vikali unyama na ukatili uliofanywa na genge la watu nchini Somalia wa kumbaka binti wa miaka 9 .

Katika taarifa iliyotolewa leo na mwakilishi maalum wa UNFPA nchini Somalia Bwana Anders Thomsen amesema ukatili huo wa kutisha umefanyika jana Mei 29 katika mji wa katikati mwa somalia wa Bulo-Burde kilometa 425 Magharibi mwa Moghadishu ambapo genge la watu lilimvamia na kumbaka msichana wa miaka 9.

Ameongeza kuwa “Tunalaani vikali kitendo hiki cha kinyama na kisistiza dhamira yetu ya kusimama pamoja na serikali na watu wa somalia kuhakikisha kwamba ukatili wa kingono na wa kijinsia unatokomezwa na kwamba wasichana na wanawake wanafurahia utu, haki zao za binadamu, usawa na wanaweza kuishi maisha huru bila hofu na ukatili katika hali zote.”

Pia amesema UNFPA iko pamoja na familia ya binti huyo na imetoa wito kwa serikali kufanya uchunguzi wa haraka wa uhalifu huo na kuhakikisha wahusika wanawajibishwa kisheria. Amehimiza kwamba “Hebu na tufanye kazi pamoja kuhakikisha upatikanaji wa hatua za ulinzi wa kutosha kwa wasichana na wanawake nchini Somalia.”

Kwa mujibu wa duru mbalimbali binti huyo hivi sasa anapatiwa matubabu hospitali , ikiwemo pia huduma ya ushauri nasaha.

TAGS:Somalia, ukatili wa kingono, UNFPA, Anders Thomsen

 

♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter