Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Taarifa kuhusu madhara ya vimbunga Msumbiji hazikuwasilishwa ipasavyo- Ripoti

Sehemu ya madhara ya kimbunga Idai katika eneo la bandari ya Beira nchini Msumbiji.
WFP/Maktaba
Sehemu ya madhara ya kimbunga Idai katika eneo la bandari ya Beira nchini Msumbiji.

Taarifa kuhusu madhara ya vimbunga Msumbiji hazikuwasilishwa ipasavyo- Ripoti

Tabianchi na mazingira

Udhaifu katika usambazaji wa taarifa  kuhusu vimbunga Idai na Kenneth nchini Msumbiji, ni moja ya sababu ya vimbunga hivyo kuwa na madhara makubwa kwa binadamu na miundombinu, imesema taarifa iliyotolewa leo mjini Beira Msumbiji na Geneva, Uswisi na shirika la hali ya hewa duniani, WMO.

Jopo la wataalamu wa hali ya hewa wa kimataifa na masuala ya maji likiloongozwa na Filipe Lúcio kutoka WMO limebaini hayo kufuatia kutumwa kwao kwenda kutathmini hali halisi na mapendekezo ya kupunguza madhara iwapo majanga kama hayo yatatokea siku za usoni.

Mathalani, jopo hilo liligundua kuwa maonyo ya mapema ya vimbunga yaliyotolewa na kituo cha shirika hilo huko Reunion yalikuwa sahihi kabisa isipokuwa tatizo lilikuwa uelewa wa hatari zitokanazo na maonyo hayo na kile ambacho kila mtu anapaswa kufanya.

“Ujumbe wa mawasiliano unapaswa kurahisishwa na ujumuishe hatari zinazoweza kutokea. Elimu na uhamasishaji kuhusu majanga vinapaswa kuwa masuala endelevu. Maonyo ya mapema yanaweza kuwa fanisi iwapo yataenda pamoja na hatua za kukabili majanga,” imesema ripoti ya jopo  hilo.

Ili kufanikisha hilo, jopo hilo limependekeza kuwa lazima kuwepo na mbinu sahihi za matumizi fanisi ya maeneo ya mabondeni ikiwemo mipango miji bora na matumizi ya ardhi.

Wakimbizi wa ndani huko Beira  nchini Msumbiji, wakianika nguo zao katika shule ya sekondari iliyotumiwa kama makazi ya muda ya manusura ya kimbunga idai mwezi Machi 2019
UNICEF/UN0291739/Prinsloo
Wakimbizi wa ndani huko Beira nchini Msumbiji, wakianika nguo zao katika shule ya sekondari iliyotumiwa kama makazi ya muda ya manusura ya kimbunga idai mwezi Machi 2019

Halikadhalika miundombinu yenye matumizi tofauti tofauti ambayo inaweza kutumiwa kama makazi wakati wa majanga na mafuriko.

WMO pia inataka kuwepo kwa mfumo mbadala wa mawasiliano pindi ule wa kawaida unaposhindwa kufanya kazi wakati wa majanga.

Akizungumzia ripoti hiyo, Katibu Mkuu wa WMO Petteri Taalas amesema,  “vimbunga hivyo viwili ni tamko la onyo kuwa Msumbiji ni lazima ijiwekee mfumo wa mnepo.”

Wataalamu hao wamependekeza uwekezaji wa takribain dola milioni 27 kwa ajili ya kuimarisha sekta ya utabiri wa hali ya hewa na masuala ya maji nchini Msumbiji, ikijumuisha ujenzi, ukarabati na uwekaji wa miundombinu ya kisasa kwenye sekta hizo.

Ripoti hiyo itawasilishwa tarehe 1 mwezi ujao wa Juni wakati wa mkutano wa kimataifa wa kuchangisha fedha kusaidia Msumbiji, mkutano utakaofanyika kwenye mji wa pwani wa Beira.