Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Tiba dhidi ya sumu ya nyoka yapatiwa muarobaini

Sumu itokanayo na kung'atwa na nyoka inaweza kuleta madhara ya kimwili na kiakili na kusababisha mtu kupoteza mwelekeo wa maisha  yake.
Thea Litschka-Koen
Sumu itokanayo na kung'atwa na nyoka inaweza kuleta madhara ya kimwili na kiakili na kusababisha mtu kupoteza mwelekeo wa maisha yake.

Tiba dhidi ya sumu ya nyoka yapatiwa muarobaini

Afya

Shirika la afya ulimwenguni, WHO limezindua mkakati wake wa kukabiliana na tatizo la watu kung’atwa na nyoka, tatizo ambalo shirika hilo limesema ni la kutisha.

Mkurugenzi wa WHO idara ya udhibiti wa magonjwa ya kitropiki yaliyosahaulika, NTD, Dkt. Mwele Malecela akizungumza mjini Geneva, Uswisi wakati wa uzinduzi amesema watu kati ya 80,000 hadi 138,000 wanafariki dunia kila mwaka baada  ya kung’atwa na nyoka kwa kuwa matibabu si rahisi kupatikana.

Amesema hali ni mbaya kwasababu tatizo hilo linapata jamii ambazo zimepuuzwa na zinazoishi maeneo yaliyo mbali kufikika, “watu wasio na uwezo wa kupata usafiri wa haraka ili kuwafikisha maeneo ambayo wanaweza kupata dawa ya kutibu sumu ya nyoka.”

Ni kwa mantiki hiyo mkakati  uliozinduliwa unalenga kuzuia na kudhibiti kitendo cha watu kuumwa na nyoka ili kupunguza kwa asilimia 50 idadi ya vifo na watu wanaopata ulemavu baada ya kuumwa na nyoka katika kipindi cha  miezi 12.

Mkakati huo una mipango inayolenga jamii zilizoathirika zaidi pamoja na mifumo yao ya afya kwa kuhakikisha kuwa wanapata tiba salama na sahihi kwa kuongeza ushirikiano na ubia katika ngazi zote.

WHO  hivi sasa inaelimisha wakazi wa Eswatini kuhusu nyoka na sumu zao na pia wanafundisha watu wanaojitolea kukamata nyoka ili kuepusha watu kung'atwa kama ilivyo  pichani.
Thea Litschka-Koen
WHO hivi sasa inaelimisha wakazi wa Eswatini kuhusu nyoka na sumu zao na pia wanafundisha watu wanaojitolea kukamata nyoka ili kuepusha watu kung'atwa kama ilivyo pichani.

Dkt. Mwele amesema jamii zinahitaji kufahamu zaidi kuhusu suala la kuumwa na nyoka na kutambua kile wanachopaswa kufanya huku mifumo ya afya nayo ikijengewa uwezo wa kushughulikia tatizo hilo.

“Katika maeneo mengi, hakuna tiba dhidi ya sumu ya nyoka. Kwa hiyo watu wanaumwa na nyoka, na hawana cha kufanya zaidi ya kwenda kwa mganga wa kienyeji na hatimaye mara nyingi wanafariki dunia na kifo chao ni cha taratibu na maumivu makali,” amesema Dkt. Mwele.

Kwa mantiki hiyo WHO inasema lengo kuu ni kuhakikisha kuwa kuna matibabu salama, sahihi na ya gharama nafuu kama vile tiba dhidi ya sumu ya nyoka na matibabu ya ziada. Shirika hilo limesema mpango huo unaenda sambamba na kuboresha na kuimarisha uzalishaji na usambazaji wa sumu ya nyoka.

Dkt. Mwele amesema kuwa “awali kulikuwepo na makundi yanatengeneza dawa ya kuondoa sumu ya nyoka. Lakini ile ari ya kutengeneza na kupungua mahitaji kwenye soko yamesababisha washindwe kuendelea kutengeneza.”

Amesema kuwa ingawa “tunajaribu kuepusha kuumwa na nyoka kwa kuvaa viatu, nugo na kadhalika, lakini bado ni lazima tuhakikishe kuwa pindi mtu anaumwa na nyoka awe ma iwezp wa kuchukua hatua badala ya kuwepo katika mazingira ya kutokuwa na dawa dhidi ya sumu ya nyoka kama ilivyo sasa.”

Ili kuondokana na hali hiyo amesema WHO itashirikiana na taasisi za utafiti ili kuhamasisha upatikanaji wa tiba mpya, mbinu za utambuzi na za kisasa za tiba ili kuboresha matibabu kwa wagonjwa walioumwa na nyoka.