Komesheni ruzuku kwa sekta ya mafuta na matumizi ya fedha za watoa ushuru kutokomeza dunia- Guterres

28 Mei 2019

Tunahitaji kutoza kodi uchafuzi wa hewa lakini sio watu na kukomesha ruzuku kwa sekta ya mafuta,  amesema Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, António Guterres hii leo Jumanne kwenye kongamano la dunia la muungano  wa R20, shirika  linaloungwa mkono na Umoja wa Mataifa lilioanzishwa na aliyekuwa gavana wa California nchini Marekani Arnold Schwarzenegger.

Katibu Mkuu akizungumza mjini Vienna, Austria amesema dhana ya kwamba kukomesha ruzuku kwa sekta ya mafuta kunaimarisha maisha ya watu si kweli kwa sababu inamaanisha "fedha za walipa kodi zinatumika kuchagiza vimbunga, kusambaza ukame na ongezeko la joto, kuyeyusha theluji na kubabua matumbawe; kuangamiza dunia.”

Bwana Guterres ametoa wito wa kuacha  ujenzi mpya wa viwanda vya  makaa wa mawe na kuchagiza matumizi endelevu na  uzalishaji akisema kwa ufupi"tunahitaji uchumi unaojali mazingira na sio unaoyasambaratisha.”

Ufadhili wa jamii inayokabiliwa na hewa ya ukaa

Kuelekea kongamano la Umoja wa Mataifa kuhusu mabadiliko ya tabianchi mwezi Septemba mwaka huu, Bwana Guterres tayari amwaeteua Rais wa Ufaransa,Waziri Mkuu wa Jamaica na Kiongozi Mkuu wa Qatar kuchagiza ufadhili kimataifa kuhakikisha lengo la dola bilioni 100 zilizokubaliwa na nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa katika kongamano la mabadiliko ya tabianchi huko Paris mwaka 2015, zinazohitajika kusongesha mbele mikakati ya kudhibiti na kukabiliana nambadiliko ya tabianchi katika dunia inayoendelea.

Katibu Mkuu huyo amesisitiza  wafadhili kuacha kuwekeza katika uchafuzi na kuimarisha biashara zinazojali mazingira na kuimarisha mikopo kwa suluhu za hewa ndogo ya mkaa. Ameongeza kwamba sekta binafsi na wawekezaji wanapaswa kuunga mkono ajenda thabiti kwa sababu sio tu kwamba hatua dhidi ya mabadiliko ya tabianchi ni faida kwa watu na sayari dunia lakini pia inaweza kuwa na faida kwa biashara.

UNEP/Jerker Tamelander
Uchafuzi wa bahari unatishia uwepo wa matumbawe ambayo ni muhimu kwa uhai wa viumbe vya baharini ikiwemo samaki

Kuna nuru gizani

Akirejelea ziara yake ya hivi karibuni visiwa vya Tuvalu kusini mwa Pacifiki ambayo huenda vikazama kutokana na kuongezeka kwa kina cha maji ya bahari, Bwana Guterres amesisitiza kwamba ni nadra kwa siku kupita bila kusikia habari za janga lingine iwe ni mafuriko, ukame, moto wa nyika au mvua kubwa.

Hata hivyo Katibu Mkuu huyo amesema kuna matumaini kwasababu licha ya kwamba hali ya sasa ni hatari sana lakini kubadilisha na kukumbatia uchumi unaojali mazingira kutakuwa na faida kubwa kwa jamii kote ulimwenguni na maji safi na hewa, uchafuzi mdogo na kilimo kisicho na kemikali na kupungua kwa kupotea kwa bayoanuai.

Kongamano la R20 ni mradi wa muda mrefu wa kusaidia kanda, mataifa na miji kutekeleza malengo ya maendeleo endelevu na kufikia malengo ya kulinda mazingira kimataifa kama ilivyoorodheshwa kwenye mkataba wa Paris wa kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.

 

 

 

Shiriki kwenye Dodoso UN News 2021:  Bofya hapa Utatumia dakika 4 tu kukamilisha dodoso hili.

♦ Na iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter