Maelfu wakimbia mashambulizi Nigeria na kuingia Niger:UNHCR

28 Mei 2019

Ongezeko la machafuko na mashambulizi  ya hivi karibuni katika baadhi ya sehemu za Kaskazini Magharibi mwa Nigeria yamewalazimisha watu takribani 20,000 kufangasha virago na kukimbilia Niger  kusaka usalama.

Kwa mujibu wa shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi UNHCR kuendelea kuzorota kwa usalama ndani ya Nigeria ni jambo linalotia hofu kubwa na linashirikiana na mamlaka ya Niger ili kutoa huduma za msingi na kuorodhesha wakimbizi wapya walioanza kumiminika tangu mwezi Aprili mawaka huu. UNHCR inasema hadi kufikia sasa wakimbizi 18,000 wameshaorodheshwa katika mchakato wa awali. Akifafanua kuhusu machafuko hayo mapya msemaji wa UNHCR mjini Geneva Babar Baloch amesema

SAUTI YA BABAR BALOCH

"Tunavyofahamu watu wamearifiwa kukimbia kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo mapigano baina ya wakulima na wafugaji na makundi ya makabila mbalimbali, tahadhari pamoja na watu kutekwa kutokana na kudai kikombozi”

Ameongeza kuwa wakimbizi waliotoka Nigeria na kuwasili katika jimbo la Maradi nchini Niger wanasimulia kushuhudia machafuko makubwa na ukatili na mashambulizi dhidi ya raia ikiwemo mashambulizi ya mapanga, kutekwa, na ukatili wa kingono na asilimia kubwa ya wakimbizi hao ni wanawake na watoto.

Jimbo la Diffa UNHCR inasema hivi sasa linahifadhi watu 250,000 wakiwemo wakimbizi kutoka Nigeria na na wakimbizi wa ndani  wa Niger.  Na kwa nchi nzima ya Niger kuna wakimbizi zaidi ya 380,000 na waoomba hifadhi wengi kutoka Mali na Nigeria japo pia imetoa hifadhi kwa watu 2,782 waliosafirishwa toka Libya wakisubiri suluhu ya muda mrefu.

Niger inaendelea kuwa mfano katika kanda kwa kutoahifadhi ya usalama kwa wakimbizi wanaotoroka vita , machafuko na ukatili mwingine katika nchi za jirani. Na imekuwa ikiacha mipaka yake wazi kwa ajili ya wakimbizi licha ya machafuko yanayoendelea katika nchi jirani za Nigeria, Mali na Burkina Faso.

 

 

♦ Kurambaza ukurasa mahsusi wa Siku ya Kiswahili Duniani bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter