Tofauti za kijamii na kitamaduni ni ‘utajiri mkubwa, si tishio’ - Antonio Guterres

27 Mei 2019

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa akizungumza hii leo Jumatatu mjini Vienna Austria akiwa na Balozi wa amani wa Umoja wa Mataifa, mwanamuziki mcheza ‘Cello’ au Fidla, Yo-yo Ma, amesema kama lilivyo kundi la muziki mzuri, jamii zilizofanikiwa zina uwiano wa utofauti na utamaduni na hicho ni chanzo cha utajiri mkubwa na si tishio.

Bwana Guterres alikuwa akizungumza dhidi ya chaguzi za mabunge ya ulaya hivi karibuni ambayo yalionesha kuongezeka kwa vyama vya siasa vinavyoelekea kujenga jukwaa zaidi la kitaifa la kupinga wahamiaji.

Bwana Guterres amewaambia wale waliokusanyika kwa ajili ya ‘siku ya vitendo’ kuwa ni muhimu “katika mjadala wa sasa wa Ulaya” kuwa na “mtizamo wa pamoja wa amani, kwa ajili ya utu wa mwanadamu, kwa ajili ya haki za binadamu” pamoja na maadili yaliyobainishwa katika mkataba wa Umoja wa Mataifa.

“Jamii za sasa zina makabila mengi, dini nyingi, utamaduni mbalimbali. Na hivyo ni utajiri si tishio. Kama ilivyo kwa kundi la muziki la wanamuziki kutoka duniani kote, wanahitaji kufanya mazoezi ili kucheza kwa usawa. Utofauti unahitaji uwekezaji ili kuhakikisha kuwa kila jamii inajihisi kuwa utambulisho wao unaheshimika kama ambavyo utambulisho wa mpoiga violini unatakiwa kuheshimika na wapiga vyombo wengine.” Ameeleza Guterres.

 

Katibu Mkuu ameeleza kuwa suala la uhamiaji linahitaji uwekezaji badala ya kuwaacha wale wanaosafirisha watu kiaharamu kupata faida kutokana na uhamiaji haramu na kuwaacha wale wanaosafirishwa wakiwa matatizoni.

Guterres pia ameongelea miaka 40 ya Umoja wa Mataifa mjini Vienna, Austria.

Akizungumza mara baada ya mkutano na Rais wa Austria Alexander Van Der Bellen, Bwana Guterres ameisifu Austria kwa kuunga mkono Umoja wa Mtaifa kwa miaka yote 40 iliyopita, na Vienna imekuwa nyumbani kwa mashirika na taasisi nyingi muhimu za Umoja wa Mataifa.

Vienna ikiwa ni moja ya Makao Makuu, Bwana Guterres amesema anashawishika kuwa kazi zinazofanyika Vienna zitasaidia kutunza amani na usalama wa dunia katika nyakati ngumu.

 

 

♦ Tafadhali iwapo unataka kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud