Kuchelewa kuondoka kwa ndege za misaada ya kibinadamu kunawaweka hatarini wahamiaji nchini Yemen.

27 Mei 2019

Taarifa iliyotolewa hii leo mjini Aden Yemen na shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulika na wahamiaji IOM inasema zaidi ya wahamiaji waethiopia wanaoshikiliwa katika hali mbaya mjini Aden Yemen ilikuwa warejeshwe nyumbani kwa msaada wa shirika hilo katika operesheni iliyopangwa kuanza jumamosi ya wiki iliyomalizika yaani Mei 25, lakini zoezi hilo limecheleweshwa na marufuku ya shughuli za ndege katika eneo hilo.

Tangu katikati mwa mwezi Aprili, mamlaka za Aden, Abyan na Lahj ziliwashikilia wahamiaji, wengi wao kutoka Ethiopia katika makambi yenye hali mbaya. Kwa takribani watu 5,000 walishikiliwa katika viwanja viwili vya michezo na kambi moja ya jeshi bila huduma muhimu. IOM imekuwa ikitoa misaada muhimu ya kuokoa maisha kama vile maji, chakula na huduma ya afya kwa watu hao.

Kama sehemu ya msaada wake kwa wahamiaji waliokwama na kwaioko hatarini, IOM hutoa msaada wa kuwarejesha katika nchi zao kupitia program ya kurejea kwa hiyari.  Katika uwanja wa 22 May mjini Aden, IOM iliwachunguza na kuwasajili wahamiaji waethiopia 2,315 wakiwemo wanawake 150 na watoto 470 ambao kwa haraka walitaka kurudi nyumbani na kuondoka katika eneo lenye mgogoro nchini Yemen.

Mkurugenzi wa operesheni na dharura wa IOM mjini Geneva Mohammed Abdiker amesema, “IOM inatoa usaidiazi wa kurejea nyumbani kuwasaidia wahamiaji wanaoshikiliwa mjini Aden na tunahitaji msaada wa jumuiya ya kimataifa kutusaidia kuwafikisha wahamiaji hawa nyumbani.”

IOM ilipata ruhusa kutoka katika mamlaka zinazohusika kuanza shughuli za kuwarejesha hadi mji mkuu wa Ethiopia, Addis Ababa kuanzia jumamosi tarehe 25 Mei, na ilipangwa kuwe na ndege moja kila siku hadi tarehe mbili mwezi Juni. Ijumaa, serikali ya Yemen na muungano wa nchi za kiarabu waliahirisha kuondoka kwa ndege ya kwanza hadi jumtano ya terehe 29 Mei.

Taarifa ya IOM inasema kuchelewa huku kunaweka hatarini usalama wa zaidi ya wahamiaji 2,300 ambao wanaendelea kushikiliwa katika hali mbaya ambazo hazikubaliki kimataifa wakiwa katika hatari ya kupata magonjwa. Mapema mwezi huu, takribani wahamiaji 14 waliokuwa wanashikiliwa huko Lahj walifariki kutokana na matatizo yanayohusishwa na ugonjwa wa kipindupindu. Katika uwanja wa michezo wa 22 Mei mjini Aden, askari wenye silaha wameendelea kuuzingira na kuweka ugumu kwa misaada ya kibinadamu.

“Maisha yamepotea kutokana na magonjwa ambayo yameletwa na kuwa katika mazingira mabaya na kijana mmoja mdogo alipigwa risasi akiwa anashikiliwa, pengine hataweza kutembea tena.” Amesema Abdiker.

 

♦ Kutembelea ukurasa maalum wa UNGA76 bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter