Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Nimejisikia vibaya sana kumpoteza mwenzangu Chitete - Koplo Omary

Koplo Ali Khamis Omary ni mlinda amani mtanzania aliyeokolewa na mlinda amani marehemu Chancy Chitete kutoka Malawi.
UNIC Dar es salaam
Koplo Ali Khamis Omary ni mlinda amani mtanzania aliyeokolewa na mlinda amani marehemu Chancy Chitete kutoka Malawi.

Nimejisikia vibaya sana kumpoteza mwenzangu Chitete - Koplo Omary

Amani na Usalama

Wiki hii kwenye makao makuu ya Umoja wa Mataifa kumetolewa tuzo ya juu zaidi ya ulinzi wa amani ya Kapteni Mbaye Diagne.

Katibu Mlkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres akikabidhi medali ya Mbaye Diagne kwa Lachel Chitete Mwenechanya, mjane wa Private Chancy Chitete, mlinda amani wa Malawi aliyeuawa huko DRC mwezi Novemba 2018 akipambana na waasi.
UN /Manuel Elias
Katibu Mlkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres akikabidhi medali ya Mbaye Diagne kwa Lachel Chitete Mwenechanya, mjane wa Private Chancy Chitete, mlinda amani wa Malawi aliyeuawa huko DRC mwezi Novemba 2018 akipambana na waasi.

Tuzo hiyo hutolewa kwa mlinda amani ambaye ameonyesha ujasiri wa kipekee wakati akiwa kwenye operesheni za ulinzi wa amani na mwaka huu wa 2019, medali hiyo imekwenda kwa Chancy Chitete, mlinda amani kutoka Malawi ambaye aliuawa tarehe 14 mwezi Novemba mwaka jana wa 2018 huko Kididiwe mjini Beni jimbo la Kivu Kaskazini nchini Jamhuri ya Kidemokrasia  ya Congo, DRC, wakati akiokoa maisha ya mlinda amani mwenzake kutoka Tanzania.

Chitete na mlinda amani huyo kutoka Tanzania Koplo Ali Khamis Omary walikuwa kwenye operesheni ya  ulinzi wa amani ya kikosi cha kujibu mashambulizi, FIB cha ujumbe wa kulinda amani wa Umoja wa Mataifa huko Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC, MONUSCO.

Medali hiyo ya Chitete ilikabidhiwa kwa mjane wake Lachel Chitete Mwenechanya ambaye aliongozana na mwanae pamoja na dada wa Chancy aitwaye Eunice Chipeta.

Mara baada ya kukabidhiwa tuzo hiyo, Eunice alizungumza na Idhaa ya Umoja wa Mataifa na kuelezea shukrani zao za dhati kwa Umoja wa Mataifa kwa kutambua mchango wa ndugu yao na kisha akasema kwamba,  “hatuchukulii hii kama jambo la kawaida kwa sababu katu hatukuwahi kutarajia kwamba tungalialikwa kwenye makao makuu ya Umoja wa Mataifa kupokea tuzo hii.”

Kisha akamzungumzia kaka yake akieleza kuwa, “naweza kusema kuwa Chitete alikuwa ni mchapakazi, kwa kuwa hii haikuwa mara yake ya kwanza kwenda kulinda amani DRC,  hii ilikuwa mara ya pili, kwa hiyo hata kama alifahamu kile ambacho kingalitokea, alijitolea kwenda ili kusaidia kwenye ulinzi wa amani ili tuwe na nchi salama ya kuishi.”

Bi. Chipeta amesema zaidi ya hapo, Chitete alikuwa ni mtu rafiki na alipenda kutembelea ndugu na jamaa zake akisema kuwa anachokumbuka ni kwamba, “kila wakati akiwa DRC alipiga simu na tulizungumza na kila mara akirejea nyumbani alikuwa anatutembelea na hilo nitakumbuka.”

Dada huyo wa Chitete akatoa shukrani zake akisema kuwa, “Ni kwa niaba ya familia ya Chitete tunahisi kuwa tumeheshimiwa sana, kile ambacho Umoja wa Mataifa imefanya imeweka familia ya Chitete na serikali ya Malawi kwenye ramani. Tutaishi tukikumbuka kumbukumbu hizi.”

Koplo Ali Khamis Omary ni mlinda amani mtanzania aliyeokolewa na mlinda amani marehemu Chancy Chitete kutoka Malawi wakati wa operesheni huko kambi ya Naru Kididiwe Masahriki mwa Congo.
UNIC Dar es salaam
Koplo Ali Khamis Omary ni mlinda amani mtanzania aliyeokolewa na mlinda amani marehemu Chancy Chitete kutoka Malawi wakati wa operesheni huko kambi ya Naru Kididiwe Masahriki mwa Congo.

Mlinda amani ambaye aliokolewa na Chitete, Koplo Omary akiwa Dar es salaam nchini Tanzania amekumbuka kile ambacho kilitokea tarehe 14 Novemba mwaka 2018.

Koplo Omary akihojiwa na Stella Vuzo wa kituo cha habari cha Umoja wa Mataifa ameenda mbali kuzungumzia mazingira ya kazi akisema kuwa mazingira ya DRC  yanafahamika kutokana na kuwa na misitu minene na ndio ilisababisha hali yaliyotoke na kisha akazungumzia mtazamo wake kuhusu ulinzi wa amani akisema kuwa bado zina umuhimu sana kwasababu matatizo bado yapo na dhumuni la ulinzi wa amani ni kuokoa watu.

Koplo Omary akatoa ujumbe wake kwa walinda amani akiwajulisha kuwa waendelee kuwa na moyo wa kufanya kazi na ushirikiano na watekeleze majukumu yao. Halikadhalika kwa raia amewaeleza kuwa wachukulie walinda amani kuwa ni watu wa kusongesha amani na hivyo wawapatie ushirikiano.

Akizungumzia alichojifunza baada ya kunusurika amesema ni uvumilivu, ushirikiano na kutekeleza majukumu unayopewa na taifa kwa umakini na ametoa wito kwa Umoja wa Mataifa kuendelea kuwapatia msaada walinda amani.