Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Dola milioni 363 zachangishwa huko Norway kukabili ukatili wa kingono kwenye mizozo

Manusura wa ukatili wa kingono akiwa Monrovia, Liberia.
UN Photo/Staton Winter
Manusura wa ukatili wa kingono akiwa Monrovia, Liberia.

Dola milioni 363 zachangishwa huko Norway kukabili ukatili wa kingono kwenye mizozo

Afya

Hii leo huko Norway, jumla ya  dola milioni 363 zzimepatikana kama ahadi kutoka mataifa 21 kwa ajili ya mipango ya kukabiliana na ukatili wa kingono na kijinsia kwenye mizozo kwa mwaka 2019, 2020 na kuendelea. Fedha hizo zimepatikana wakati wa mkutano wa aina yake  ulioleta pamoja maafisa wa ngazi ya juu kutoka mataifa 90 pamoja na Umoja wa Mataifa .

Norway ndio mwenyeji wa mkutano huo wa kwanza kabisa wenye maudhui ya kibinadamu na kujikita kwenye kukabili ukatili wa kingono kwenye mizozo ambapo inashirikiana na serikali za Iraq, Somalia, Falme za kiarabu na Umoja wa Mataifa sambamba na kamati ya kimataifa ya msalaba mwekundu, ICRC.

Washiriki wote walikubaliana kuwa ukatili wa kingono na kijinsia kwenye mizozo unaweza kuzuiwa.

Mathalani Mkurugenzi Mtendaji wa shirika la Umoja wa Mataifa  la kuhudumia watoto, UNICEF Henrietta Fore amezugnumzia umuhimu wa hatua salama katika harakati zote za utoaji wa misaada ya kibinadamu akitaka ushiriki zaidi wa mashirika ya wanawake na mipango mipya bunifu ya kumaliza zahma hiyo ya ukatili wa kingono na kijinsia kwenye mizozo.

Mkutano wa kutokomeza ukatili wa kingono na kijinsia uliofanyika Oslo, Norway 24 Mei 2019
OCHA
Mkutano wa kutokomeza ukatili wa kingono na kijinsia uliofanyika Oslo, Norway 24 Mei 2019

Ametaja ukatili kama vile ukatili wa kingono, ndoa za umri ndogo, ujauzito katika umri mdogo, vipigo na unyanyasaji akisema kuwa "kwa mamilioni ya wasichana walionaswa kwenye majanga ya kibinadamu, vitendo hivyo si vigeni. matukio haya ya kila siku yanawaweka wanawake kwenye hatari maradufu katika mazingira yasiyo na uhakika  ya udharura."

Bi. Fore ametaka wahudumu wa kibinadamu walio mstari wa mbele hadi watendaji wa serikali sambamba na mashirika ya Umoja wa Mataifa na yale ya kiraia yachukue hatua za dharura kwa kuwa hali si nzuri.

Hata hivyo amewapongeza kwa ujasiri wao na azma yao ya kuhakikisha kuwa wanaondokana na ghasia ambazo zimewazuia kwenda shule, kusaka ajira na hata kusaidia wanawake na wasichana wengine ambao wamekumbwa na maisha magumu.

"Ingawa wamekumbwa na ukiukwaji mkubwa wa haki, bado hawajakubali kile walichopia ndio kiendeshe maisha yao, bali azma yao ndio inawaongoza," amesema Bi. Fore

Akizungumzia ukatili wa kingono, Waziri wa Mambo ya nje wa Norway, Ine Eriksen Soreide amesema “unafanyika maeneo mbalimbali duniani, ukiathiri wanawake, wasichana, wanaume na wavulana. Kwa pamoja tunatoa wito wa kuongezwa kwa utashi wa kisiasa na usaidizi wa kifedha. Tunahitaji hatua thabiti dhidi ya  tatizo hili la kibinadamu ambalo mara nyingi linapuuzwa, halipatiwi fedha za kutosha na wakosaji wanakwepa sheria.”

Naye Mkurugenzi Mtendaji wa shirika la Idadi ya watu la Umoja wa Mataifa Dkt. Natalia Kanem amesema, “jamii ya kimataifa inapaswa kuchukua hatua zaidi kusaidia manusura wa ukatili wa kingono na watu walio hatarini kukumbwa na zahma hiyo, sambamba na kumaliza tabia ya watekelezaji wa vitendo hivyo kukwepa sheria.

Awali ukatili wa kingono na wa kijinsia kwenye mizozo ulichukuliwa kama matokeo ya vita lakini hivi sasa unatambuliwa kama silaha na uhalifu wa vita.