Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Chonde chonde El Salvador jizuieni msamaha kwa wakiuka haki za binadamu:Bachelet

Janet akiwa karibu na mchoro wa kaburi aliouchora kuonesha majonzi yake kutokana na kumpoteza mtoto wake aliyekuwa na umri wa miaka 17 aliyeuawa na kundi la uhalifu huko El Salvador kwa kuwa hakukubali kujiunga nao.
UNHCR/Marta Martinez
Janet akiwa karibu na mchoro wa kaburi aliouchora kuonesha majonzi yake kutokana na kumpoteza mtoto wake aliyekuwa na umri wa miaka 17 aliyeuawa na kundi la uhalifu huko El Salvador kwa kuwa hakukubali kujiunga nao.

Chonde chonde El Salvador jizuieni msamaha kwa wakiuka haki za binadamu:Bachelet

Haki za binadamu

Mswada wa awali uliowasilishwa kwenye Bunge la El salvador ukitaka kufutwa kwa hukumu za vifungo kwa watu waliokiri kutekeleza uhalifu wakati wa vita vya silaha nchini humo na badala yake kuwapa adhabu ya huduma kwa jamii , ofisi ya haki za binadamu ya Umoja wa Mataifa inasema mswada huo ukipitishwa utawafaidisha waliotekeleza uhalifu dhidi ya binadamu na hautotenda haki kwa waathirika.

Katika taarifa yake iliyotolewa leo, Kamishina Mkuu wa ofisi ya haki za binadamu Michelle Bachelet amesema rasimu ya mswada huo wa masuala ya haki na maridhiano hivi sasa inajadiliwa bungeni nchini El Salvador na ina vipengee kadhaa ambavyo vinaweza kutafsriwa kama ni msamaha usiostahili.

Ameongeza kuwa “mswada huo kwa hakika unafaidisha wahalifu, wapangaji wa uhalifu huo na viongozi wa juu ambao wakati wa vita walitoa amri au walishindwa kuchukua hatua za kuzuia au kukomesha uhalifu dhidi ya ubinadamu na uhalifu wa kivita kama vile mauaji ya kiholela ya watoto, wanawake na wazee, watu kutoweshwa , utesaji, ukatili wa kingono na ukiukwaji mwingine wa sheria za kimataifa.”

Kamishina mkuu anahoji mswada huo wa karibuni ambao msingi wake ni kazi ya tume ya haki za binadamu kwa sababu baadhi ya wajumbe wake walihusika kwenye vita vya silaha  na pia kutokana na kutokuwepo uwazi na ushiriki wa waathirika wakati wa mafunzo.

Amesisitiza kuwa “inatia hofu kwamba mswada huu mpya unatokana na kazi ya tume  hii bila kujumuisha mtazamo wa waathirika, hususani wale ambao wanaishi katika jamii za vijijini na ambao sauti zao hazijasikika hadi sasa na pia wale ambao wameshuhudia athari za vita .” Tume ilianzishwa kutokana na uamuzi wa mahakama kuu ambayo Julai mwaka 2016 ilitangaza sheria ya msamaha kwa kuibadilisha sheria ya mwaka 1993 ambayo haikuzingatia katiba na kulitaka Bunge kuandaa muswada mpya wa sheria ya kitaifa ya maridhiano.

Bachelet amezitaka taasisi imara kudhihirisha umuhimu wa mchakato wa masuala ya mpito ya haki nchini El Salvador na umuhimu wa kuendelea kusonga mbele kuelekea ukweli, haki, msamaha na hakikisho la kutorejea kwa hali kama hii kwa ajili ya maridhiano ya kitaifa. “ofisi yangu inarejea kusisitiza kwamba iko tayari kutoa msaaza wa kiufundi kwa Bunge na taasisi zingine kwa ajili ya suala hili.”