Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Guterres ataja mambo matatu ili kuimarisha ulinzi wa raia kwenye mizozo

Walinda amani wanawake kutoka Tanzania wanaofanya kazi na kikosi cha kujibu mashambulizi, FIB cha Ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini Jamhuri ya kidemokrasia ya Kongo, DRC, MONUSCO katika eneo la Beni, Mavivi jimbo la kivu Kaskazini.
©MONUSCO/FIB/Mohammed Mkumba
Walinda amani wanawake kutoka Tanzania wanaofanya kazi na kikosi cha kujibu mashambulizi, FIB cha Ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini Jamhuri ya kidemokrasia ya Kongo, DRC, MONUSCO katika eneo la Beni, Mavivi jimbo la kivu Kaskazini.

Guterres ataja mambo matatu ili kuimarisha ulinzi wa raia kwenye mizozo

Amani na Usalama

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa leo limekuwa na mjadala wa wazi kuhusu ulinzi wa raia kwenye mizozo ambapo Katibu Mkuu Antonio Guterres amesema kadri giza linavyozidi kutanda katika ulinzi wa raia kwenye mizozo, ni lazima kuweka na kutekeleza kanuni za kuimarisha ulinzi.

Akihutubia Baraza hilo mjini New York, Marekani, Guterres amesema miaka 20 tangu chombo hicho kipitishe azimio la kulinda raia bado hali ni tete licha ya mafanikio yaliyopatikana kwenye baadhi ya maeneo.

Mathalani ametaja mafanikio hayo kuwa ni pamoja na “ulinzi wa watoto dhidi ya ukatili wa kingono umeimarishwa kwa kujumuishwa kwa washauri maalum kwenye ujumbe wa ulinzi wa amani. Utoaji wa taarifa na ufuatiliaji wa ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu na ushirikiano na pande kinzani umesababisha watoto wengi kuondoka kwenye vikundi vya kujihami na kujumuishwa na familia zao.”

Kama hiyo haitoshi, huko Sudan Kusini, azimio la Baraza la Usalama limewezesha takribani wakimbizi wa ndani 200,000 wapatiwe hifadhi kwenye vituo salama.

Ujumbe wa kulinda amani wa Umoja wa Mataifa nchini Sierra Leone, (UNAMSIL) miaka 20 iliyopita ulikuwa na jukumu mahsusi wa kulinda raia. (picha ni ya mwaka 2006)
UN /Eric Kanalstein

Hata hivyo amesema bado hali ni tete si tu kwa raia bali pia watoa huduma za kibinadamu akinukuu ripoti yake iliyowasilishwa mbele ya Baraza la Usalama ikisema kuwa mwaka 2018 pekee, watu 22,800 katika nchi sita pekee waliuawa na kujeruhiwa katika mizozo. Nchi hizo ni Afghanistan, Iraq, Mali, Somalia, Sudan Kusini na Syria.

Katika mizozo hiyo, “pindi silaha za milipuko zinapotumika kwenye maeneo yenye idadi kubwa ya watu, asilimia 90 ya wanaouawa au kujeruhiwa ni raia.”

Kama hiyo haitoshi, Katibu Mkuu amesema wahudumu wa afya nao hawajaachwa kwa kuwa “ghasia dhidi yao na wahudumu wa afya na vituo vya huduma imeendelea. Shirika la afya ulimwenguni, WHO limesema kumekuwepo na matukio 705 ya mashambulizi dhidi ya watumishi hao na vituo vya afya katika mizozo minane tu iliyosababisha vifo vya watu 451 na majeruhi 860.”

Katibu Mkuu amesema changamoto kuu ni kuhakikisha sheria za kibinadamu za kimataifa zinaheshimiwa kwenye mizozo akisema baadhi ya maeneo pande kinzani zinaheshimu ilihali kwingineko mwenendo wa kuheshimu kanuni hizo unapaswa kuhojiwa.

Nchini Sudan Kusini, mlinda amani wa Umoja wa Mataifa akishiriki maonyesho ya sanaa kwenye mji mkuu Juba kuhusu jinsia na ukatili wa kingono na kijinsia. (Picha ya Mei 2019)
UNMISS\Nektarios Markogiannis
Nchini Sudan Kusini, mlinda amani wa Umoja wa Mataifa akishiriki maonyesho ya sanaa kwenye mji mkuu Juba kuhusu jinsia na ukatili wa kingono na kijinsia. (Picha ya Mei 2019)

Kwa mantiki hiyo amenukuu mapendekezo matatu kwenye ripoti yake ili kuweza kulinda raia kwenye mizozo ambapo mosi ni kuanzisha mifumo ya wazi wa kitaifa yenye sera ambazo zinaanzisha taasisi na wajibu wa kulinda raia kwenye mizozo.

Pili ushirikiano wa dhati na mashirika ya misaada ya kibinadamu ili kulinda raia kwenye mizozo na tatu kuhakikisha wahusika wa ukatili dhidi ya raia kwenye mizozo wanawajibishwa na ndipo amesema “Baraza la Usalama linaweza kuchukua hatua zaidi kusaidia ikiwemo usaidizi wa kifedha na kiufundi kwenye uchunguzi na kufikisha mbele ya sheria watekelezaji wa uhalifu wa kivita.”

Hata kama ni vigumu wenyewe kuelewana, basi muwe wawazi kwenye maamuzi yenu- ICRC

Punde baada ya Katibu Mkuu kumaliza hotuba yake, Rais wa shirikisho la vyama vya msalaba mwekundu, ICRC Peter Maurer akapatiwa fursa ya kuzungumza akisema kuwa, “siyo tu maamuzi ya wanachama wote wa Umoja wa Mataifa hususan wajumbe wa Baraza la Usalama ni muhimu, lakini pia ukosefu wa maamuzi ya Baraza hili nao unatesa raia.”

Amesema katika uwanja wa vita, ambako ICRC inafanya kazi, mara nyingi pande kinzani zinatumia ukosefu wa maridhiano baina ya wajumbe wa Baraza la Usalama kama fursa ya kusongesha operesheni zao za kijeshi bila ukomo au hofu yoyote ya kuwajibishwa.

Bwana Maurer amesema, “miaka 70 baada ya kupitishwa kwa kauli moja kwa mikataba ya Geneva, na zaidi ya miaka 40  baada ya itifaki za nyongeza kwenye mikataba ya Geneva, na miaka 20 baada ya azimio la Baraza la Usalama kuhusu ulinzi wa raia, bado tunashuhudia ukiukwaji mkubwa kila uchao.”

Ameongeza kuwa, “ingawa tunaelewa kuwa maridhiano ya kisiasa ni magumu, tunawaomba muwe wazi kuhusu msaada wenu katika kuheshimu sheria za kibinadamu za kimataifa katika kutaja na kufuatilia kuwa hakuna mtu yoyote aliye juu ya sheria na hakuna raia yeyote anayepaswa kuenguliwa kwenye ulinzi.”

Mkuu huyo wa ICRC amesema kuwa “wakati tunawaomba ninyi wajumbe wa Baraza la Usalama na jamii ya kimataifa kwa ujumla, tunaomba basi angalau msizuie watu wenye uhitaji ambao wanahaha wao wenyewe kujilinda.”