Chama cha wanawake cha misaada ya kisheria Côte d’Ivoire chajitosa kuwasaidia wasio na utaifa.

Mwanaume huyu anayefahamika kwa jina Oumar ambaye alikuwa katika hatari ya kukosa uraia, akionesha kadi ya baba yake aliyoipta enzi za ukoloni wa ufaransa.
UNHCR/Hélène Caux
Mwanaume huyu anayefahamika kwa jina Oumar ambaye alikuwa katika hatari ya kukosa uraia, akionesha kadi ya baba yake aliyoipta enzi za ukoloni wa ufaransa.

Chama cha wanawake cha misaada ya kisheria Côte d’Ivoire chajitosa kuwasaidia wasio na utaifa.

Haki za binadamu

Kutokuwa na utaifa ni moja ya changamoto kubwa inayowakabili sio tu wahamiaji, bali pia wakimbizi, waomba hifadhi, watu waliotawanywa na majanga na hata waliozaliwa katika nchi ambazo sheria haziwaruhusu kuwa na utaifa kama wazazi wao si raia. Kufuatia wito wa Umoja wa Mataifa wa kukabiliana na changamoto hii katika kila nchi na kuhusisha wadau wote zikiwemo asasi za kiraia hatua zimeanza, mathalani nchini Côte d’Ivoire  ambako wataalamu wa misaada ya kisheria kutoka Chama cha misaada ya kisheria cha wanawake wanafanya kampeni dhidi ya tatizo la kukosa utaifa Kijiji hadi Kijiji ili kuwaelimisha watu jinsi ya kupata nyaraka za kisheria zinazoeleza haki zao. 

Kouassi Adjo Rosine, ni miongoni mwa wanasheria wa Chama hicho anasema,“tunawaorodhesha, na kuchukua taarifa zao zote ili waweze kutambuliwa, ikiwa ni pamoja na jina la baba na mama, tarehe zao za kuzaliwa, taarifa zote.”

Kuna sababu mbalimbali za uwepo wa watu wasio na utaifa nchini Côte d’Ivoire. Baadhi ni wahamiaji wa kihistoria kutoka katika nchi nyingine na kwa hivyo hawana asili ya Côte d’Ivoire ili watumie kama kigezo cha kupewa utaifa kwa mujibu wa sheria.

Lakini maelfu ya wengi ni watu wenye asili ya hapo hapo Côte d’Ivoire ispokuwa ni kwasababu hawana nyaraka za kuthibitisha uraia wao. Mchakato wa kupata nyaraka za utaifa unaweza kuwa wa gharama kubwa, mgumu, unaochukua muda mrefu na unaotegemea maamuzi ya jaji. Wengi wanaweza hata wasijaribu. Bila uthibitisho wa uraia wanaishi bila ulinzi wa kisheria na hawana haki ya kupata elimu ya juu, ajira rasmi au umiliki wa mali. Siloué Ngolo ni mmoja wa watu  wasio na utaifa, anasema, “ninaogopa. Sikupata karatasi zangu-ninaweza kusafiri kwenda wapi? Nitizame. Mimi ni mzee. Kujaribu kukimbia huku na kule kupata nyaraka zangu inaweza kuwa vigumu kwangu. Lakini kama ningekuwa nazo, kwa umri wangu, ingekuwa vema, kwasababu watoto wangu wangekuwa nazo kama wangezihitaji.”

Chama cha misaada ya kisheria cha wanawake wa Côte d’Ivoire kinawapatia watu taarifa kuhusu haki zao na mwongozo wa kuchukua hatua ikiwemo kwa watoto waliozaliwa maeneo ya vijijini au pembezoni. Familia nyingi zimevuka kipindi cha miezi mitatu cha kutangaza kupata mtoto ili wapate cheti cha kuzaliwa moja kwa moja. Wataalamu wa misaada ya kisheria wanawahamasisha kukutana na kutia saini pamoja nao kisha kupeleka maombi rasmi katika mahakama ili kuharakisha mchakato.