Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Muundo mpya wa sheria za dawa Afrika Magharibi wawasilishwa huko Geneva

Mgonjwa kiwa na sampuli ya vidonge.
UNICEF/Olivier Asselin
Mgonjwa kiwa na sampuli ya vidonge.

Muundo mpya wa sheria za dawa Afrika Magharibi wawasilishwa huko Geneva

Afya

Mkutano wa Baraza Kuu la shirika la afya ulimwenguni, WHO, ukiendelea huko Geneva, Uswisi, kamisheni ya dawa kwa nchi za Afrika Magharibi, pmoja na ile ya kimataifa kwa kushirikiana na shirika la kukabiliana na Ukimwi la Umoja wa Mataifa, UNAIDS,leo wamewasilisha mfumo bora wa sheria za dawa kwa ukanda huo wa Afrika.

Mfumo huo umewasilishwa kwa mawaziri wa afya wa nchi wanachama wa jumuiya ya Afrika Magharibi, ECOWAS kwa lengo la kuhakikisha kuwa sheria zozote kuhusu dawa siyo tu zinadhibiti matumizi bali pia zinaangazia ubinadamu mathalani kwa watumiaji wa madawa ya kulevya na wanaoishi na Virusi Vya Ukimwi, VVU.

Hatua hiyo inazingatia ukweli  kwamba sheria kuhusu dawa hizo huko Afrika Magharibi bado hazijawa na tija ambapo si matumizi ya madawa au usafirishaji wa madawa ya kulevya umepunguzwa kwa kutumia sheria zilizopo.

Imeelezwa kuwa usafirishaji madawa ya kulevya kwenye ukanda huo umefikia kiwango cha kutishia utulivu huko Afrika Mgharibi takwimu zikionesha kuwa tangu mwaka 2014, kiwango cha matumizi ya bangi ni cha juu ikilinganishwa na kiwango cha dunia.

Akizungumza kwenye kikao hicho, Rais wa zamani wa Nigeria Olusegun Obasanjo ambaye pia ni Mwenyekiti wa kamisheni ya dawa ya Afrika Magharibi amesema, “ongezeko la watu wanaotiwa korokoroni wakisubiri kufikishwa mahakamani kwa makosa yahusianano ya madawa yamesababisha kufurika kwa magereza,”

Amesema, “watu wanaotumiwa madawa ya kulevya wanahitaji tiba na si kuadhibitiwa. Kuwanyanyapaa na kuwasweka rumande kunazidi kuathiri afya zao na kuweka shinikizo zaidi katika mifumo ya mahakama ambayo tayari imezidiwa uwezo.”

Ni kwa mantiki hiyo mfumo  uliowasilishwa unatoa mwongozo wa nchi kuupokea na kufanyia marekebisoh sheria zao za dawa, kwa kuzingatia wajibu wao wa kisheria kimataifa.

Muundo huo unaweka mfumo au kiwango ambacho si haramu kwa mtu kutumia au kukutwa na madawa ya kulevya na vile vile mtu huyo kuruhusiwa kupata huduma za afya na msaada.

Halikadhalika unatambua vikwazo ambavyo vinapaswa kuondolewa ili mamilioni ya watu wanaohitaji huduma za afya ikiwemo wale wanaoishi na saratani au virusi vya Ukimwi waweze kupata tiba watakayo.

Akiwasilisha muundo huo, mbele ya mawaziri wa afya, Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa UNAIDS Gunilla Carlsson amesema, “ nchi zinatakiwa kuzingatia mtazamo wa kibinadamu kuhusu VVU na matumizi ya madawa ya kulevya ili kuhakikisha kuwa afya na ustawi wa binadamu ndio unapatiwa kipaumbele.”

“Tunatambua kuwa utumiaji wa madawa ili kupunguza maumivu unafanya kazi, tunatambua kuwa kutoharamisha matumizi ya madawa kunafanya kazi, nchi haziwezi kuendelea kupuuza ushahidi huu na hivyo zichukue  hatua haraka,” amesema Bi. Carlsson.

UNAIDS inasema kuenea kwa unyanyapaa, ubagzi na ghasia dhidi ya watu maskini ambao wanajidunga madawa ya kulevya kunawaghubika pia na kiwango kikubwa cha maambukizi ya VVU.

Kwa mantiki hiyo wanasisitiza utashi wa kisiasa wa kuanza kutumia muundo mpya wa sheria za dawa ili kushughulikia mzigo wa sasa wa maambukizi ya magonjwa kwenye maendeleo.