Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Tatizo la mataifa mengi kuhusu maendeleo ni mipango-Dkt Mukhisa Kituyi

Mukhisa Kituyi, Katibu Mtendaji wa Kamati ya biashara na maendeleo ya Umoja wa Mataifa, UNCTAD wakati wa mahojiano na Idhaa ya Kiswahili ya Umoja wa Mataifa.
UNnewskiswahili/Patrick Newman
Mukhisa Kituyi, Katibu Mtendaji wa Kamati ya biashara na maendeleo ya Umoja wa Mataifa, UNCTAD wakati wa mahojiano na Idhaa ya Kiswahili ya Umoja wa Mataifa.

Tatizo la mataifa mengi kuhusu maendeleo ni mipango-Dkt Mukhisa Kituyi

Ukuaji wa Kiuchumi

Shida kubwa ya nchi zinazotegemea rasilimali za ndani ya nchi ni mpangilio usio mzuri wa vipaumbele wakati bei za bidhaa inapokuwa nzuri.

Kauli hiyo imetolewa na Katibu mkuu Mtendaji wa Kamati ya Umoja wa Mataifa ya biashara na maendeleo, UNCTAD, Dkt. Mukhisa Kituyi katika mahojiano maalum na Idhaa ya Kiswahili kandoni mwa mkutano wa uchangishaji fedha kwa ajili ya maendeleo endelevu mapema mwezi huu.

Ripoti iliyotolewa na Umoja wa Mataifa mapema mwezi huu wa Mei inasema idadi ya mataifa yanayotegemea rasilimali za ndani imeongezeka kutoka 92 kati ya mwaka 1998 na 2002 na kufikia 102 kati ya mwaka 2013 na 2017 ambapo Dkt Mukhisa Kituyi anasema rasilimali zingesaidia iwapo kungekuwa na mipango mizuri.

Sauti ya Dkt Kituyi

“Kwa muda mrefu tumekuwa sisi (UNCTAD) tumekuwa tukiongoza ulimwengu wote katika kampeni ya kuhamasisha umma kuhusu shida walizonazo wanaotegemea rasilimili katika mataifa yao. Lakini shida moja tuliyonayo ni kwamba mataifa yanayotegemea sana rasilimali, wakati bei ya kimataifa inapopanda wanasahau kuwa bei hii inaweza kushuka sasa matumizi saa nyingine yanazidi kuliko ambavyo wangewekeza kwa siku zijazo, na sasa bei ya rasilimali inapopungua ndipo wanaanza kupata madeni, madeni yanaongezeka.”

Na sasa nini kifanyike Dkt Kituyi anafunguka

Sauti ya Dkt Kituyi

“Pengine ni vizuri wakati wa shida kama sasa wana shida za kulipa madeni, huu ndio wakati wa kusema kuwa kama rasilimali zinauzwa kwa bei nafuu na bei zaidi kimataifa, huu ni wakati wa kupunguza madeni, siyo wakati wa kuagiza vitu vikubwa, kuwekeza kwenye miradi ambayo hamuwezi kuimaliza mpaka wakati rasilimali bei inashuka na kuanza kuwa maskini tena. Haya ndiyo tunajaribu kuwaeleza na kuwaonesha vile wengine walivyojaribu kujimudu wanapokuwa na shida kama zenu.”

 

TAGS: UNCTAD, Mukhisa Kutuy