Sera thabiti zahitajika kupata matunda ya kupanda miti karibu na mimea-FAO

20 Mei 2019

Upandaji miti sio suala la kuchagua kati ya misitu na kilimo bali unapaswa kupata msaada wa kisera unaohitajika, limesema shirika la chakula na kilimo duniani, FAO leo huko Montpellier, Ufaransa.

Akizungumza katika kongamano la nne duniani kuhusu kilimo mchanganyiko wa mazao ya kawaida na misitu, Naibu Mkurugenzi mkuu wa FAO, Maria Helena Semedo amesema mfumo wenye sera thabiti unaweza kuendeleza uzalishaji wa chakula na kutoa faida za kiuchumi na kimazingira kwa ajili ya watumiaji wa ardhi katika ngazi zote.  

Kilimo hicho kinachojumuisha mazao ya kawaida au mifugo na misitu kinapata umaarufu kutokana na uwezo wa kukabiliana na hewa chafuzi na mabadiliko ya tabianchi pamoja na kuimarisha ukuaji kijamii, kiuchumi na kimazingira kwa ajili ya maendeleo vijijini.

FAO imesema ujumuishaji wa miti na mazao kwa makusudi unaweza pia kuchangia katika kuhifadhi bayoanuai.

Bi. Semedo amesema uimarishaji wa kilimo cha mazao ya kawaida na misitu ni lengo la miradi kama vile muongo wa Umoja wa Mataifa wa kilimo cha familia. Aidha ameongeza kwamba leo ikiwa siku ya nyuki duniani, miti hunufaisha nyuki na viumbe wavushaji na kuongeza mazao kwa asilimia 24.

FAO imesema iko tayari kuunga mkono juhudi za nchi wanachama kujumuisha kilimo cha mazao na misitu kwenye sera kwa ajili ya kufikia malengo ya maendeleo endelevu, SDGs.

Kongamano hilo limewaleta pamoja watendaji wa sekta ya kilimo cha aina hiyo, watafiti, viongozi wa biasahra na mashirika ya kiraia kutoka takriban nchi 100.

 

 

Shiriki kwenye Dodoso UN News 2021:  Bofya hapa Utatumia dakika 4 tu kukamilisha dodoso hili.

♦ Na iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter