UNMISS yazuru jamii ya Lobonok kutathmini haki za binadamu Sudan Kusini

20 Mei 2019

Timu ya Ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini Sudan Kusini, UNMISS imezuru jamii ya Lobonok kwenye jimbo la Jubek eneo la Equatoria, kusini mwa Sudan Kusini kwa ajili ya kutathmini hali ya haki za bindamu kwa wakazi wa eneo hilo. 

 

Msafara huo wa timu ya ujumbe wa UNMISS ukielekea eneo la Lobok kukutana na wenyeji. Wenyeji nao wako tayari kusikia mazuri waliyokuja nayo, hali ya mgeni njoo mwenyeji apone, kwani madhila waliyoyapitia wakazi ni ya kusikitisha kama asimuliavyo mkazi huyu wa eneo hili akisema "ninateseka kama mwanamke, sisi sote hatuna furaha kwa sababu bibi yetu mmoja amebakwa na vijana wawili. Hili linanifanya kulia kwa sababu bibi yetu anateseka. Mtu mmoja amefariki dunia kutokana na tukio hilo.”

Kutiwa saini kwa makubaliano ya amani yaliyoboreshwa, kumechangia kupunguza vurugu za kisiasa kote nchini Sudan  Kusini. Hata hivyo mapigano ya mara kwa mara yanaendelea katika baadhi ya maeneo, kusini mwa nchi,  huku wakazi katika eneo la Lobonok wakitoa mfano wa tukio lililohusisha vikosi vilivyojihami ambavyo vilipora mali na kutekeleza vitendo vya ukatili wa kingono. Laku Simon ni  chifu wa eneo la Karpeto ambaye anasema kuwa “mli zetu zote zilichukuliwa na jeshi wakisema kwamba wanakuja hapa kutulinda lakini sasa ni tofauti. Wameharibu Kijiji chetu, sasa kijiji kizima kimesalia upweke. Watu wachache waliosalia ni kwasababu yangu, la sivyo wote wangeshaondoka.”

Kwa sasa hali ni tulivu huku waliokimbia mwaka jana wakirejea kuangalia hali ya usalama na kupanda mimea, Annie Rashidi-Mulumba, ni afisa wa haki za binadamu, UNMISS anafafanua kuwa « kwa ujumla hata wahudumu wa kibnadamu wanarejea, na hilo linawajengea imani raia na wakazi na maisha yanaendelea kama mnavyoona. Watu wanapita kwa uhuru zaidi, wanawake na watoto na maduka yamefunguliwa, hiyo ni ishara nzuri kwa Lobonok iklinganishwa na hali mwezi Februari wakati watu wengi walifurushwa kwa sababu ya vurugu eneo hili. »

Kwa sasa matumani ni kwamba kurejea kwa wakulima na familia zao kutasaidia eneo hilo kuendeleza sifa yake ya kuwa mzalishaji wa lishe Sudan Kusini kwa kuzalisha chakula kingi kwa ajili ya watu wake na jamii zingine nchini kote.

 

♦ Tafadhali iwapo unataka kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud