Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mtaalam maalum wa UN Sudan alaani matumizi ya nguvu dhidi ya waandamanji

Waandamanaji wakiandaman nje ya makao makuu ya vikosi vilivyojihami vya Sudan katika mji mkuu, Khartoum.
UN Sudan/Ayman Suliman
Waandamanaji wakiandaman nje ya makao makuu ya vikosi vilivyojihami vya Sudan katika mji mkuu, Khartoum.

Mtaalam maalum wa UN Sudan alaani matumizi ya nguvu dhidi ya waandamanji

Amani na Usalama

Mtaalam wa maalum wa Umoja wa Mataifa wa haki za binadamu nchini Sudan Aristide Nononsi, amelaani matumizi ya nguvu kupita kiasi dhidi ya waandamanaji wiki hii wanaosaka mapinduzi yanayoongozwa na raia nchini humo, huku ripoti zikisema kwamba watu takriban sita waliuawa na wengine 100 walijeruhiwa.

Kwa mujibu wa taarifa iliyochapishwa kwenye wavuti wa Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya haki za bindamu, OHCHR, mnamo tarehe 13 mwezi huu wa Mei, askari wa vikosi visivyojulikana wakiwa wamevalia sare za vikosi vya utoaji msaada wa haraka walitumia risasi za moto dhidi ya waandamanaji kwenye mji mkuu  Khartoum na kusababisha vifo vya watu sita ikiwemo afisa wa jeshi.

Aidha ripoti zinasema siku mbili baadaye vikosi hivyo vilifyatua risasi za moto dhidi ya waandamanaji waliokuwa wakijaribu kutoa vizuizi barabarani kuelekea makao makuu ya jeshi.

Nononsi ametoa wito kwa baraza la kijeshi la mapinduzi kuzingatia wajibu wao kulinda waandamanaji wa amani nchini Sudan na kuwaacha waelezee maoni yao na wasiwasi wai kuhusu mustakabali w anchi yao kupitia njia za amani. 

Aidha ametoa wito kwa vikosi vya uhuru na mabadiliko kuhakikisha maandamano ya amani na kuepukana na vurugu.

Bwana Nononsi ametoa wito kwa pande zote kurejelea mazungumzo ili kuhakikisha ukabidhi wa mamlaka kupitia mchakato unaoongozwa na raia katika kipindi cha siku 60 kwa mujbu wa Muungano wa Afrika na pendekezo la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa.

Halikadhalika mtaalam huyo ameelezea utayari wake wa kushirikiana na pande husika kuunda taifa ambalo matakwa muhimu ya watu wasudan yanazingatiwa na haki za binadamu zinaheshiniwa pamoja na sheria.