Warohingya zaidi ya 250,000 wapata vitambulisho wengi kwa mara ya kwanza:UNHCR
Warohingya zaidi ya 250,000 wapata vitambulisho wengi kwa mara ya kwanza:UNHCR
Zaidi ya wakimbizi warohingya 250,000 kutoka nchini Myanmar sasa wameorodheshwa na serikali ya Bangladesh na shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi UNHCR, na kupatiwa vitambulisho
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa leo na UNHCR wakimbizi warohingya wanaohifadhiwa nchini Bangladesh hawana utaifa. Licha ya kuishi nchini Myanmar kwa vizazi na vizazi warohingya walipoteza uraia wao kufuatia mabadiliko ya sharia ya mwaka 1982 nchini Myanmar.
Shirika hilo linasema zaidi ya wakimbizi warohingya 900,000 wanabanana kwenye makazi ya Cox’s Bazar nchini Bangladesh huku 741,000 miongoni mwa wakimbiz hao walikimbia Myanmar Agosti 2017.
Akifafanua kuhusu hatua hiyo ya kuwapa vitambulisho wakimbizi hao msemaji wa UNHCR mjini Geneva Andrej Mahecic anasema, “zoezi la usajili lililoanza Juni 2018 ni la kulinda haki ya wakimbizi warohingya ili waweze kurejea nyumbani Myanmar kwa hityari katika siku za usoni.Hadi sasa serikali na UNHCR wamesajili wakimbizi 270,348 kwenye makazi ya wilaya ya Cox’s Bazar. Kila siku Zaidi ya wakimbizi 40,000 wanasajiliwa katika maeneo sita ambako zaidi ya wafanyakazi 450 wanafanya kazi kwa saa nyingi kwa lengo la kukamilisha mchakato baadaye mwaka huu 2019.”
Vitambulisho wanavyopewa wakimbizi vina taarifa muhimu kama picha zao, majina , tarehe za kuzaliwa na mahali walipozaliwa, vitambulisho hivyo pia vinasema kuwa Myanmar ndio nchi walikotoka na wanaopatiwa vitambulisho ni wakimbizi wote walio na umri wa miaka 12 na kuendelea.
UNHCR inasema zoezi la usajili ni muhimu kwa lengo la kuboresha takwimu za wakimbizi nchini Bangladesh na pia kutoa taswira kamili kwa serikali na mashitrika ya kimataifa ya misaada na kuwafanya kuelewa idadi na mahitaji ya wakimbizi hao. Pia takwimu hizo zitasaidia mipango na kulenga misaada kwa wahusika wanaoihitaji zaidi hususan wanawake, Watoto na watu wenye ulemavu.