Hala-hala wageni mnaokuja Tanzania mifuko ya plastiki marufuku

16 Mei 2019

 

Katika kutekeleza lengo la Umoja wa Mataifa la kutunza mazingira, nchi wanachama zinaendelea kubuni mikakati mbalimbali ya kuhifadhi mazingira  na hali ya hewa kwa ujumla kwa kupiga marufuku uzalishaji na utumiaji wa taka ngumu zikiwemo mifuko ya plastiki.

Miongoni mwa nchi hizo ni Tanzania ambayo leo imeutangazia umma ndani ya nchi na nje kuwa kuanzia tarehe Mosi ya mwezi ujao wa Juni, mifuko yote ya plastiki haitaruhusiwa kutumika.

Taarifa iliyotolewa leo na ofisi ya Makamu wa Rais nchini humo ikiwalenga watu waanaopanga kusafiri kuelekea Tanzania, imesema, “mifuko yote ya plastiki bila kujali unene wake  itapigwa marufuku kuanzia siku hiyo tajwa, kuingia, kusafirishwa nje, kuzalishwa, kuuzwa, kuhifadhiwa kusambazwa na kutumika Tanzania bara.”

Hata hivyo tarifa hiyo imefafanua kuwa vifungashio vya dawa, bidhaa za viwandani, ujenzi, sekta ya kilimo, vyakula, na kudhibiti taka, havijapigwa marufuku hata kama vimetengenezwa kwa plastiki.

“Kutakuwa na dawati maalumu katika njia zote za kuingia Tanzania ili kuzikusanya plastiki zote ambazo wageni wanaweza kuwa wamekuja nazo nchini”, imeeleza sehemu ya tarifa hiyo ambayo tayari imewatahadharisha wageni wote kuhakikisha hawabebi mifuko ya plastiki wanapopanga safari zao za kutembelea Tanzania.

Mifuko ya plastiki inayofahamika kama ‘ziploc bags’ ambayo hutumika kubebea vitu vidogovidogo vya kujisafi wakati wa safari haikupigwa marufu kwa kuwa inategemewa itabaki kuwa mali ya mgeni na hakuna mahali popote atakapoiacha nchini Tanzania.

Taarifa hiyo imeendelea kufafanua kuwa, “serikali haikusudii kuwafanya wageni wakute usumbufu wakati wanapowasili au kuwepo  nchini wakati huu tunapotekeleza marufuku ya plastiki. Hata hivyo serikali inategemea kuwa katika kuunga mkono juhudi za kulinda mazingira na kuiweka nchi yetu katika usafi na uzuri, wageni wetu  wataukubali usumbufu mdogo unaotokana na marufu yetu ya mifuko ya plastiki.”

 

♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter