Iweje utake kuendelea kula nyama ilhali ukijua uzalishaji wake unaharibu sayari dunia?
Iweje utake kuendelea kula nyama ilhali ukijua uzalishaji wake unaharibu sayari dunia?
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres ambaye bado yuko ziarani nchini Fiji leo amekuwa na shughuli mbalimbali ikiwemo kuhutubia bunge la nchi hiyo, kuwa na mkutano wa pamoja na Waziri mkuu pamoja na kuzungumza na wanafunzi wa Chuo Kikuu cha South Pacific mjini Suva.
Katika mjadala wa maswali na majibu na wanafunzi hao wa ChuoKikuu, Katibu Mkuu amerejelea suala la hatua dhidi ya mabadiliko ya tabianchi.
Amesema “niko hapa kueleza jinsi ambavyo sisi wa kizazi cha sasa ambao tunapitisha maamuzi tunahitaji msaada wenu katika kudhibiti mazingira kwa sababu tumeshindwa kufanya vyema kazi yetu Mabadiliko ya tabianchi yanakwenda kasi kuliko kasi yetu.”
Katibu Mkuu amerejelea vile ambavyo kiwango cha joto katika miaka minne iliyopita kimekuwa cha kuliko wakati wowote ule , huku utoaji wa hewa chafuzi ya ukaa ikiongezeka akisema kuwa tayari wataalamu wanataka kutokuwepo kwa utoaji wa hewa chafuzi ifikapo mwaka 2050.
“Tatizo utoaji wa hewa chafuzi bado unaongezeka, bali inakuwa mbaya kabisa, ukame unaongezeka, theluji inayeyuka, matumbawe yanabadilika rangi na kuwa meupe, na utashi wa kisiasa unazidi kutuanguka. Kile tulichokubaliana Paris hakitekelezwi,” amesema Guterres akisema hatuko kabisa kwenye mwelekeo.
Amesema tunachotakiwa ni kubadili kabisa mwelekeo, akihoji, “bado tunajenga mitambo ya makaa ya mawe na wale wa kizazi changu hawatekelezi wajibu wao.”
Amehoji iweje mtu utake kuendelea kula nyama ya ng’ombe ukifahamu kuwa ufugaji unachochea kwa kiasi kikubwa utoaji wa hewa chafuzi zinazoongeza kiwango cha joto duniani.
Amesema matumaini yake ni kwa vijana kote duniani kuwaeleza watu wazima kuwa hamtendi mema kwa kuharibu sayari ambayo ni makazi yetu ya baadaye.
Katibu Mkuu amewapongeza vijana kwa harakati zao za kusaka ushawishi wao kutambulika na kusikika akisema kwa kuwa kizazi cha watu wazima kimeshindwa basi vijana wasimame kidete kuwaeleza watu wazima kile cha kufanya na lengo ni kupunguza kiwango cha joto kwa nyuzi joto 1.5 na hivyo “na nawategemea sana kizazi chenu kiweze kutusadia kizazi chetu kuwa na tabia njema zaidi.”
Mapema akizungumza kwenye mkutano na waandishi wa habari akiwa ameambatana na Waziri Mkuu wa Fiji, Josaia Voreqe Bainimarama, Katibu Mkuu amesema, “tunahitaji kutambua kuwa hatuko kwenye mwelekeo sahihi wa kushinda vita dhidi ya mabadiliko ya tabianchi, hata hatuko kwenye mwelekeo wa kutekeleza mkataba wa Paris wa mabadiliko ya tabianchi. Tunahitaji zaidi utashi wa kisiasa ambao utatuwezesha kubadili mwelekeo ili tuweze kuokoa sayari yetu na hakuna pahala bora ambako wameonyesha hatua kama hapa Pasifiki.”