Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mtoto 1 kati ya 7 duniani kote huzaliwa na uzito mdogo kupindukia- Ripoti

Nchini Papua New Guinea mtoto akiwa amevaa kifaa cha rangi ya chungwa kuonyesha kuwa mwili wake hauwezi kuhimili kiwango cha baridi. Hapa ni katika wadi ya watoto wachanga waliozaliwa na uzito mdogo.
UNICEF/Kate Holt
Nchini Papua New Guinea mtoto akiwa amevaa kifaa cha rangi ya chungwa kuonyesha kuwa mwili wake hauwezi kuhimili kiwango cha baridi. Hapa ni katika wadi ya watoto wachanga waliozaliwa na uzito mdogo.

Mtoto 1 kati ya 7 duniani kote huzaliwa na uzito mdogo kupindukia- Ripoti

Afya

Takwimu mpya zilizotolewa leo na watafiti kutoka mashirika ya Umoja wa Mataifa na Chuo cha tiba za kitropiki na afya cha London, Uingereza zimeonyesha kuwa mwaka 2015 zaidi ya watoto milioni 20 walizaliwa duniani kote wakiwa na uzito wa chini kupindukia, ambao ni chini ya kilo mbili na nusu au pauni 5.5

Kiwango hicho ni mtoto 1 kati ya watoto 7 ambapo takribani asilimia 75 ya watoto hao walizaliwa katika nchi za Asia ya Kusini na zile za Afrika zilizo kusini mwa jangwa la Sahara.

Tatizo ni kubwa kwa nchi zilizoendelea pia

Hata hivyo watafiti hao wanaojumuisha wale wa shirika la afya duniani, WHO, shirika la kuhudumia watoto UNICEF na Chuo hicho Kikuu cha London, wamesema bado tatizo la watoto kuzaliwa na uzito mdogo ni la juu kwenye nchi za kipato  cha juu barani Ulaya, Amerika Kaskazini, Australia na New Zealand.

Wamesema katika maeneo hayo hakuna hatua madhubuti zimechukuliwa tangu mwaka 2000 kupunguza tatizo la watoto kuzaliwa na uzito mdogo, wakizingatia utafiti wao uliohusisha mataifa 148 na vizazi hai milioni 281,  utafiti ambao umechapishwa katika jarida la masuala ya afya la Lancet.

Hatua hizo hazijachukuliwa, ingawa kwamba mwaka 2012, mataifa yote 195 wanachama wa WHO waliazimia kupunguza kwa asilimia 30 idadi ya watoto wanaozaliwa na uzito mdogo ifikapo mwaka 2025 wakilinganisha na viwango vya mwaka 2012.

Je wafahamu vichocheo vya mtoto kuzaliwa na uzito mdogo?

Watafiti hao wanasema kwa kuzingatia takwimu za sasa ni vyema kuchukua hatua kukabili vichocheo vya watoto kuzaliwa na uzito mdogo.

Vichocheo hivyo ni mwanamke kubeba ujauzito akiwa na umri mkubwa, kubeba ujauzito mfululizo, magonjwa ya shinikizo la damu wakati wa ujauzito, maambukizi kama magonjwa ya malaria, lishe duni, mjamzito kukumbwa na uchafuzi wa hali ya hewa, matumizi ya tumbaku na madawa ya kulevya.

Mtoto akiwa amebebwa na mamamke katika kituo cha afya nchini Mali.
UNICEF/UN0186355/Njiokiktjien
Mtoto akiwa amebebwa na mamamke katika kituo cha afya nchini Mali.

Bila kufahamu uzito wa mtoto anapolizwa, kuwalinda itakuwa ndoto

Pamoja na hatua za kudhibiti vichochezi, watafiti hao wanataka kila serikali itimize ahadi hasa ile ya kuhakikisha kuwa kila mtoto anayezaliwa anapimwa uzito na huduma za kliniki zinaimarishwa.

“Kila mtoto mchanga anayezaliwa anapaswa kupimwa uzito, lakini duniani hatuna takwimu za uzito kwa takribani theluthi moja ya watoto wachanga,” amesema Julia Krasevec, mtaalamu wa takwimu na ufuatiliaji kutoka UNICEF

Amesema kuwa “hatuwezi kusaidia watoto waliozaliwa na uzito mdogo bila kuboresha wigo na usahihi wa takwimu tunazokusanya,” amesema Bi. Krasevec.

Mifumo bora itasaidia nini?

Amesema kuwa iwapo kutakuwepo na mifumo bora ya kukusanya takwimu, wanaweza kuwa na uzito sahihi wa mtoto wakiwemo wale wanaozaliwa majumbani na hivyo kutoa huduma bora zaidi kwa watoto wachanga na mama zao.

Zaidi ya asilimia 80 ya watoto milioni 2.5 duniani wanaofariki dunia kila mwaka wanakuwa wamezaliwa na uzito mdogo kwasababu wanakuwa wamezaliwa kabla ya wakati.

Watafiti hao wamesema mtoto anayezaliwa na uzito mdogo ambao wanaishi wana hatari kubwa ya kudumaa au kupata matatizo ya kukua kimwili na kupata magonjwa kama vile kisukari na moyo iwapo hawatapata matunzo bora.