Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ugonjwa wa kupoteza kumbukumbu unaathiri watu milioni 50 kote ulimwenguni, WHO yatoa mwongozo wa kupunguza hatari

Bibi kizee akiendesha baiskaeli nchini Croatia (13 Februari 2013). Mwongozo mpya wa WHO unasisitiza mazoezi ili kujikinga na ugonjwa wa kupoteza kumbukumbu.
World Bank/Miso Lisanin
Bibi kizee akiendesha baiskaeli nchini Croatia (13 Februari 2013). Mwongozo mpya wa WHO unasisitiza mazoezi ili kujikinga na ugonjwa wa kupoteza kumbukumbu.

Ugonjwa wa kupoteza kumbukumbu unaathiri watu milioni 50 kote ulimwenguni, WHO yatoa mwongozo wa kupunguza hatari

Afya

Shirika la afya ulimwenguni WHO leo limetoa mwongozo mpya wa kusaidia watu kupunguza hatari za ugonjwa wa kupoteza kumbukumbu, ambao pamoja na mambo mengine unataja masuala kama vile kufanya mazoezi mara kwa mara, kutovuta sigara, kuepuka matumizi hatarishi ya vileo na lishe bora.

Akizungumza katika uzinduzi wa mwongozo huo mjini Geneva Uswisi hii leo  Dkt. Neerja Chowdhury, Mkurugenzi mkuu katika kitengo cha afya ya akili na matumizi ya mihadarati, WHO amesema kwa sasa kuna wagonjwa takriban milioni 50 wa kupoteza kumbukumbu kote ulimwenguni idadi hii ikitarajiwa kuongezeka mara tatu ifikapo mwaka 2050

Amesema ugonjwa wa kupoteza kumbukumbu sio tu unaathiri mgonjwa lakini pia familia yake, walezi na una gharama za kiuchumi kwa jamii, ikitarajiwa kwamba ifikapo mwaka 2030 gharama hiyo itafikia dola trilioni 2 kila mwaka.

WHO inasema kwamba watu walio na ugonjwa huo wanakabiliwa na hatari ya kunyanyapaliwa kutokana na ukosefu wa taarifa na kwa sababu hakuna tiba kwa sasa WHO inasisitiza umuhimu wa kuzuia ambapo muongozo unalenga

(Sauti ya Chowdhury)

“Kile ambacho tunahimiza nchi kufanya ni kujumuisha mbinu za kupunguza hatari za ugonjwa wa kupoteza kumbukumbu kwenye sera na mipango, kuwa na programu za kutoa mafunzo kwa wahudumu wa afya ili waweze kutoa mapendekezo hayo kwa watu ambao wanatembelea kliniki zao na kama tulivyosema katika muongozo huu kuna haja ya kufanya utafiti zaidi na tunahimiza serikali kuwekeza katika sio tu tiba lakini pia kuzuia, kupunguza hatari na matibabu mujarabu kwa watu walio na ugonjwa wa kupoteza kumbukumbu.”

Ugonjwa wa kupoteza kumbukumbu unasababisha mtu kupoteza uwezo wa kuelewa, unaathiri kumbukumbu, mawazo, uwezo wa kujifunza, lugha na unatokana na baadhi ya magonjwa au majeraha ambayo yanaathiri ubongo.