Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Nuru ya amani yamulika mji wa Kapoeta nchini Sudan Kusini

Katika picha hii kutoka maktaba, Ronda, (kulia) mmoja wa wakimbizi wa ndani akifua nguo zake kwenye kituo cha kufadhi raia huko Wau Sudan Kusini.
UNICEF/Ohanesian (maktaba)
Katika picha hii kutoka maktaba, Ronda, (kulia) mmoja wa wakimbizi wa ndani akifua nguo zake kwenye kituo cha kufadhi raia huko Wau Sudan Kusini.

Nuru ya amani yamulika mji wa Kapoeta nchini Sudan Kusini

Amani na Usalama

Ujumbe wa ngazi ya juu wa Umoja wa Mataifa umekuwepo kwenye mji wa Kapotea jimbo la Namorunyang  nchini Sudan Kusini kwa lengo la kuimarisha ujenzi wa amani na hatimaye wakazi wake waliokimbia kutokana na mapigano waweze kurejea.

 

Ukiongozwa na Mwakilishi maalum wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa nchini Sudan Kusini, David Shearer, ujumbe huo ulilenga kusaidia harakati za maridhiano na ujenzi wa mani pamoja na kupatia uhai mkataba mpya wa amani.

Wawakilishi kutoka pande zote kinzani kwenye mzozo Sudan Kusini zilishiriki ikiwemo jeshi la serikali, kikundi cha Sudan People Liberation Army upande wa upinzani, na mashirika ya kiraia na viongozi wa kidini.

Na ndipo Bwana Shearer ambaye pia ni mkuu wa ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini Sudan Kusini, UNMISS akasema kitendo cha mji wa Kapoeta kupatia kipaumbele suala la maridhiano ni jambo muhimu akisema,  “na kwangu mimi ni jambo la kutia moyo kuona watu kila pahala wanaeleza uongozi wao kuwa wanataka amani, wanataka kuona ustawi. Amani inaleta ustawi, ustawi unaleta ajira na maendeleo ya kiuchumi na huduma zote. Ni msingi wa kila kitu kwa hiyo mjadala huu wa amani ni muhimu sana.”

Kwa upande wake Gavana wa Kapoeta Louis Lobong Lojore amesema kujenga imani mashinani ni msingi wa utekelezaji wa mkataba wa amani akisema, “kuleta pande mbili kinzani pamoja hususan makamanda wa SPLA upande wa upinzani na wale wa serikali na kuwa na uwezo wa kubadilishana mawazo ni muhimu. Hii itarahisisha mawasiliano na maelewano.”

Baadhi ya waathirika wa mgogoro wa Sudan Kusini
UNMISS/Isaac Billy
Baadhi ya waathirika wa mgogoro wa Sudan Kusini

Mkutano huo umehudhuriwa pia na wawakilishi wa kamisheni ya pamoja ya kijeshi ya kusitisha mapigano ikijumuisha maafisa wa jeshi la serikali na upande wa upinzan na Meja Jenerali Isaac Moro ni mjumbe,  “kuleta amani ni jambo moja, kuendeleza amani ni jambo jingine. Kuleta amani ni lazima kulegeza msimamo lakini kuendeleza amani ni lazima ujitoa sadaka. Lazima ujitoe sana ukiwa kiongozi au mwananchi ili kuendeleza amani.”
 

Kapoeta imekuwa na utulivu na amani hivi karibuni licha ya uwepo wa vikosi vya kijeshi kutoka pande zote.

Hata hivyo uhaba wa muda mrefu wa chakula na maji umeendelea kuwa tatizo na unazuia watu wengi kuamua kurejea mjini humo ili kuendelea na maisha yao.