Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

WHO yalaani shambulizi la gari la wagonjwa Tripoli

Daktari katika matibabu ya mtoto wa umri wa miaka minne nchini Libya ambapo yaelezwa kuwa mzozo ukiendelea hosptiali zinakabiliwa na mzigo mkubwa.
WHO
Daktari katika matibabu ya mtoto wa umri wa miaka minne nchini Libya ambapo yaelezwa kuwa mzozo ukiendelea hosptiali zinakabiliwa na mzigo mkubwa.

WHO yalaani shambulizi la gari la wagonjwa Tripoli

Amani na Usalama

Shirika la afya ulimwenguni, WHO limelaani vikali shambulio dhidi ya gari la wagonjwa kwenye mji mkuu wa Libya, Tripoli ambalo limejeruhi wahudumu watatu wa afya, mmoja wao hali yake ikiwa mbaya zaidi.

Mwakilishi wa WHO nchini Libya Dkt. Syed Jaffar Hussain amesema, “shambulio hili dhidi ya gari la wagonjwa lililokuwa na nembo zote kudhihirisha kuwa linahudumia wagonjwa, ni la kusikitisha na ni ukiukwaji mkubwa wa sheria za kimataifa za kibinadamu.”

Taarifa ya WHO iliyotolewa leo mjini Tripoli imemnukuu akisema kuwa, “si tu kwamba shambulio hili limesababisha majeruhi kwa wahudumu wetu muhimu, bali pia gari lenye la wagonjwa limetekwa na hivyo kuwanyika wagonjwa huduma za siku za usoni.”

WHO inasema tangu mapigano kwenye mji mkuu  Tripoli yapambe moto kuanzia mwezi uliopita wa Aprili, magari 11 ya kusafirisha wagonjwa yameathirika mengine yameshindwa kufanya kazi kabisa kutokana na kushambuliwa huku wahudumu wa afya nao wakishambuliwa.

Mathalani taarifa hiyo imesema tarehe 3 ya mwezi uliopita, wahudumu watatu wa afya waliuawa mjini Tripoli na kwamba wahudumu waokozi walio mstari wa mbele wamekuwa wakihaha kufikia majeruhi bila wao wenyewe kujeruhiwa.

“Mapigano hayo yakiwa yameingia mwezi wa pili tangu yaanze upya, zaidi ya watu 400 wameuawa na wengine zaid iya 2000 wamejeruhiwa,” imesema WHO.

Akizungumzia kile kinachoendelea Libya hivi sasa cha miundombinu ya afya kushambuliwa,  Mkurugenzi wa WHO kanda ya Mediteranea Mashariki, Dkt. Ahmed Al-Mandhari amesema, “ukiukwaji huu wa kanuni za msingi za vita unaweza kuharibu operesheni za hospitali mashinani na timu za usafirishaji wagonjwa na hivyo kuzuia kazi zinazofanywa na wahudumu wetu wa afya waliojitolea kwa dhati ya kuokoa maisha ya watu.”

Amesema WHO katu haiwezi kukubali kitendo chochote ambacho kinaweka hatarini wahudumu wa afya na kwamba “wahudumu wa afya nchini Libya wanafanya kazi ya kuokoa maisha na hivyo ni lazima waruhusiwe kufanya kazi yao bila hatari ya ziada ya usalama au ustawi wao.”

WHO imekuwa ikiendelea kutoa huduma za afya mashinani kwa kusaidia hospitali zilizo kwenye eneo la mapigano na imepeleka dawa, vifaa vya tiba na timu za madaktari.