Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Gharama ya uagizaji chakula kupungua 2019, lakini Afrika haitonufaika

Nyama au chakula kilichopikwa kwa mkaa kina ladha tamu zaidi
UNIC/Stella Vuzo
Nyama au chakula kilichopikwa kwa mkaa kina ladha tamu zaidi

Gharama ya uagizaji chakula kupungua 2019, lakini Afrika haitonufaika

Ukuaji wa Kiuchumi

Gharama ya uagizaji wa chakula duniani kwa mwaka huu wa 2019 itapungua kutokana na ongezeko la uzalishaji wa bidhaa, imesema ripoti mpya ya makadirio ya chakula iliyotolewa leo na shirika la chakula duniani, FAO.

Ripoti hiyo ambayo hutolewa mara mbili kwa mwaka imesema gharama za uagizaji wa chakula utapungua kwa dola trilioni 1.4 ambazo ni sawa na asilimia 2.5 ikiliganishwa na mwaka uliotangulia.

Hata hivyo ripoti hiyo imesema wanufaika wa kupungua  huko kwa gharama ni nchi tajiri ilhali kwa nchi za Afrika zilizo kusini mwa jangwa la Sahara gharama inatarajiwa kuongezeka.

Ingawa ripoti pia inaonyesha kuwa kwa kupungua kwa gharama, chakula kingi zaidi kinaweza kuagizwa, hali hiyo haihusishi nchi zenye kipato cha chini zinazokabiliwa na uhaba wa chakula, ambazo pia thamani ya sarafu zao inapungua dhidi ya dola ya Marekani ambayo ndio inatumika katika miamala ya kimataifa.

“Gharama za uagizaji kahawa, chai, kakao na viungo inakadiriwa kupungua kwa karibu asilimia 50 lakini gharama ya kuagiza sukari na nafaka itasalia kama ilivyo,” imesema ripoti hiyo.

Hata hivyo habari ni njema kwa nchi maskini ni kwamba bei ya mafuta yatokanayo na mboga inatarajiwa kupungua.

Ripoti hii pia imeangazia athari za ugonjwa wa nguruwe katika uzalishaji wa nyama hiyo, biashara yake na pia kwa biashara ya aina nyingine ya nyama kama ng’ombe na kuku.

“Ugonjwa huo wa homa ya nguruwe, ASF umeenea sana China ambako ndio inazalisha nusu ya nyama yote ya nguruwe duniani, na hii itakuwa na madhara kwenye biashara ya nyama hiyo duniani na pia kwa soko la nyama na chakula cha mifugo,” imesema ripoti hiyo.

Ripoti imesema ugonjwa huo utapunguza kwa asilimia 20 uzalishaji wa nyama ya nguruwe China ikimaanisha ni fursa kwa wafugaji wa Ulaya na Marekani.

Halikadhalika, kupungua kwa uzalishaji wa nyama ya nguruwe China ina maana ya kupungua kwa uagizaji wa maharagwe ya soya ambayo hutumiwa kwenye chakula cha nguruwe.