Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Bila msaada mamia ya majeruhi wa maandamano Gaza hatarini kukatwa viungo:UN

(Maktaba) Mtoto akilia wakati mhudumu wa afya akimsogelea kutibu jeraha lake, Ni katika hospitali ya Al-Shifa mjini Gaza
UNICEF/Eyad El Baba
(Maktaba) Mtoto akilia wakati mhudumu wa afya akimsogelea kutibu jeraha lake, Ni katika hospitali ya Al-Shifa mjini Gaza

Bila msaada mamia ya majeruhi wa maandamano Gaza hatarini kukatwa viungo:UN

Msaada wa Kibinadamu

Mamilioni ya dola yanahitajika kwa ajili ya ufadhili wa msaada wa dharura Gaza ili kuokoa viungo vya takribani watu 1,700 ambao walijeruhiwa vibaya wakati wa maandamano dhidi ya Israel yaliyofanyika karibu na uzio wa mpaka wa Gaza na Israel, amesema leo afisa wa Umoja wa Mataifa wa masuala ya kibinadamu.

Akitoa ombi la dola milioni 20 kwa ajili ya kusaidia watu walioumia wakati wa mandamano hayo makubwa ya marejeo ambayo yalikuwa yakifanywa kila wiki na raia wa Gaza tangu mwaka jana na kuwaacha watu 29,000 wakijeruhiwa wengi wao na risasi za moto, Jamie McGoldrick mratibu wa masuala ya kibinadamu wa Umoja wa Mataifa kwenye eneo linalokaliwa la wapalestina amesema , rasilimali zaidi zinahitajika haraka.

Na kuongeza kuwa “Mifumo ya afya iko katika hali mbaya sana na ndio maana tumetoa ombi hili la dola milioni 20 ili kushughulikia mahitaji ya watu hao 1700, lakini pia kusaidia mfumo wa afya. Kati ya watu hao 29,000 watu 7000 wamepigwa risasi za moto na hao ndio wamekuwa wakipatiwa matibabu kwenye vituo ambayo viko katika shinikizo kubwa”

Hadi kufikia leo McGoldrick amesema viungo 120 vimekatwa tangu kuanza kwa maandamano hayo, huku watoto 20 wakiwa miongoni mwa watu  waliokatwa viungo.

Kukimbizana na wakati

Akizungumza na waandishi wa Habari mjini Geneva Uswis hii leo mratibu huyo amesema “tunakimbizana na wakati kwa baadhi ya visa hivi na athari za maambukizi ya magonjwa ya mifupa itakuwa janga kubwa, tunahitaji kutibu haraka na kuzuia hali hiyo la sivyo tutalazinmika kuwakata viungo. Utaalamu wa madaktari unaohitajika katika eneo hilo kuweza kuwatibu majeruhi 1,700 haupo.

Na kufuatia machafuko ya mwishoni mwa wiki kwenye mpaka baina ya Israel na Gaza Bwana McGoldrick amesisitiza kwamba kuna haja ya majadiliano kushughulikia hali mbaya ya kiuchumi na kibinadamu.

Pia amethibitisha kwamba mratibu maalumu wa Umoja wa Mataifa kwa ajili ya mchakato wa amani ya Mashariki ya Kati Nicolay Mladenov alikuwa Cairo ili kusisitiza kuhusu mkataba wa usitishaji uhasama kufuatia hali tete ya Gaza katika mjadiliano yaliyosimamiwa na Misri na kuongeza kuwa anatumai hilo litaruhusu misaada ya kibinadamu kuanza kupelekwa, kwa sababu “tulikuwa tunakataliwa kufanya kazi yetu kutokana na kutokuwepo na utulivu na usalama.”

Waandamanaji wakitembea kuelekea katika eneo la kukusanyika katika uzio wa Gaza
UNifeed Video
Waandamanaji wakitembea kuelekea katika eneo la kukusanyika katika uzio wa Gaza

 

Ukata wa ufadhili

McGoldrick amesema hivi leo familia ya kawaida Gaza ina deni la wastani wad ola 4000 wakati mishahara ni wastani wa dola 400 kwa mwezi. Na hali imekuwa mbaya zaidi kutokana na kiwango cha juu cha vijana kutokuwa na ajira na ukweli kwamba ombi la Umoja wa Mataifa la misaada ya kibinadamu kwa ajili ya Gaza ambalo n idola milioni 350 kwa ajili ya mwaka 2019 limefadhiliwa asilimia 14 pekee.

Na ukata huo unakumba mashirika mbalimbali yanayotoa msaada kwenye eneo linalokaliwa la wapalestina likiwemo shirika la mpango wa chakula duniani WFP ambalo limesema fedha linazohitaji kwa ajili ya kuwasaidia watu 193,000 kwenye Ukanda wa Gaza na Ukingo wa Magharibi tangu Januari mwaka huu hazijapatikana.

Na WFP inasema kwa kutoa kipaumbele katika operesheni zake kuwasaidia kwanza wanaohitaji zaidi msaada  na kwa sababu ya ukata ,hivi sasa watu 27,000 kwenye Ukingo wa Magharibi hawapatiwi msaada tena tangu Januari Mosi 2019 huku wengine wanapokea asilimia 80 tu ya kile wanachostahili kupokea kila mwezi ambacho n idola 8 badala ya dola 10.