WHO yaja na mpango mpya wa chanjo dhidi ya Ebola.

8 Mei 2019

Jopo la ushauri wa kimkakati kwa Shirika la Afya Duniani WHO kuhusu masuala ya chanjo, SAGE, limetoa mapendekezo mapya katika kushughulikia changamoto wanazokumbana nazo katika kukabiliana na mlipuko wa Ebola nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC.

Kwa muda mrefu moja ya changamoto kuu imekuwa ni wananchi kuipokea huduma ya chanjo kwa mashaka.

Mapendekezo ni pamoja na kupitisha marekebisho ya uendeshaji ambayo yanafanya kwa kasi mchakato wa chanjo na kurekebisha kipimo cha dozi kulingana na data ya ufanisi unaopatikana.

Jopo hilo pia limependekeza kuongeza idadi ya watu wanaostahili kupatiwa chanjo ya rVSV-ZEBOV-GP, kuanzisha jaribio la ziada la chanjo, kuimarisha jitihada zinazoendelea za kuwafundisha wauguzi, madaktari na wanafunzi wa udaktari kutoka katika jamii zilizoathirika na Ebola ili waje kujiunga na wafanyakazi wanaohusika na chanjo. Dialo Fatima Tabatuli ni kiongozi wa timu ya chanjo ya WHO..

(Sauti ya  Dialo Fatima Tabatuli)

“Kabla ya kuendelea na shughuli zetu za chanjo, tunahitaji kupata ruhusa ya watu wa eneo hilo ili watuambie kwanza kuwa tunapokelewa na pia kutuambia mahali pa kuweka kituo chetu. Pia ni lini tunaweza kuanza na pia kuwa tunaheshimu sheria zinazohitajika.”

Dialo Fatima anasema kila siku ya chanjo inahitaji maandalizi mengi lakini kwa chanjo ya Ebola nchini DRC, maandalizi ni mengi zaidi na chanjo inaokoa maisha japo bado changamoto zingalipo..

(Sauti ya Dialo Fatima Tabatuli)

“Ndiyo, kila kazi ina changamoto zake kama vile kuwafanya watu waelewe kuwa ugonjwa huo ni wa kweli na ili klindwa dhidi ya ugonjwa huo unahitaji kuchanjwa. Hata kama tunafahamu kuwa haitakuwa kwa asilimia mia moja. Hayo ni mambo mengi kukabiliana nayo kama kwa mfano uvumi ambao watu wanaupata kuhusu chanjo. Lakini kabla ya kuja hapa tunahitaji kutoa ufafanuzi wa wa kutosha na kuwamamasisha wat una ikiwa wanakubali, kwa kuwa hatukumalzimisha mtu wana uhuru wa kukubali n ani hiyari. Na pia hakuna anayelipwa ili kuchanjwa kwa hivyo ni hiyari yao kutoa ruhusa kabla hatujafanya lolote katika eneo lao”

Chanjo ya  rVSV-ZEBOV-GP imeshawafikia watu 111,000 tangu mlipuko mpya wa Ebola ulipotangazwa mwezi Agosti 2018.

 

♦ Tafadhali iwapo unataka kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud