Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

WFP yafanikiwa kufikia kinu cha kusaga nafaka cha bahari ya Shamu Yemen

Nafaka zilizohifadhiwa huko Dhubab, jimbo la Taiz nchini Yemen. WFP kwa muda mrefu ilikuwa imeshindwa kufikia nafaka iliyokuwa imehifadhiwa kwenye kinu cha kusagisha unga cha Red Sea na hivyo kutia shaka pengine itakuwa imeoza
Giles Clarke/OCHA
Nafaka zilizohifadhiwa huko Dhubab, jimbo la Taiz nchini Yemen. WFP kwa muda mrefu ilikuwa imeshindwa kufikia nafaka iliyokuwa imehifadhiwa kwenye kinu cha kusagisha unga cha Red Sea na hivyo kutia shaka pengine itakuwa imeoza

WFP yafanikiwa kufikia kinu cha kusaga nafaka cha bahari ya Shamu Yemen

Msaada wa Kibinadamu

Shirika la Umoja wa Mataifa la mpango wa chakula WFP na timu ndogo ya mafundi  wa kampuni ya kusaga nafaka ya bahari ya Shamu ambayo ni muhimu katika usambazaji wa chakula kwa mamilioni ya watu nchini humo, wamefanikiwa kufikakwenye kinu hicho mwishoni mwa juma na sasa wanaendelea na shughuli ya kusafisha na kukarabati mitambo au mashine kwa ajili ya maandalizi ya kuanza kusaga tena ngano na kusambaza kwa wahitaji.

WFP inasema “tutahitaji wafanyakazi zaidi na timu ya wataalam kwenda kwenye kampuni hiyo haraka, kupeleka vifaa vinavyohitajika kwa ajili ya timu inayofanya kazi kwa sasa, na ili kufanikisha hili tunahitaji kuendelea kupata fursa ya kufika kiwandani katika eneo ambalo tunajua ni nyeti na karibu na uwanja wa mapambano.”

Mpango wa WFP ni kuacha timu ndogo ya wataalam na baadhi ya wafanyakazi wa kampuni hiyo ya kusaga nafaka ili waendelee na kazi ya kusafisha vinu na kupuliza dawa kwenye ngano iliyokaa humo kwa muda mrefu.

Shirika hilo linasema zoezi hili litachukua muda wa wiki kadhaa na ndio awamu ya pili kufufua kampuni hiyo ya usagishaji nafaka na kupata unga wa ngano ambao utasafirishwa kwenye kwenye jamii nyingi za Wayemen ambazo zinahitaji msaada haraka.

WFP inasema “uhitaji wa msaada hasa wa chakula kwa Yemen ni mkubwa sana na kwa sasa kwa vile tuna timu katika eneo hilo ni muhimu sana tufanye haraka iwezekanavyo  kupata unga wa ngano na kuwapelekea wale wanaouhitaji zaidi.”

Mwezi Machi WFP iligawa chakula kwa zaidi ya watu milioni 10.6 nchini Yemen ikiwa ni idadi kubwa zaidi kuwahi kufikiwa katika muda wa mwezi mmoja.

Na kuanzia jana Mei 6 naibu mkurugenzi mtendaji wa WFP Amir Abdulla  yuko Yemen kwa ajili ziara ya siku tatu ambapo ametembelea eneo la Aden na kukutana na serikali inayotambulika kimataifa na kisha ameelekea Sana’a ambako anakutana na mwakilishi maalum wa Umoja wa Mataifa nchini Yemen Martin Griffiths, na baadaye waziri mkuu na makamu wa Rais. Kabla ya kuondoka Jumatano pia atakutana na wafanyakazi wa WFP.