Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Watu 7400 hung’atwa na nyoka kila siku, WHO yachukua hatua

WHO  hivi sasa inaelimisha wakazi wa Eswatini kuhusu nyoka na sumu zao na pia wanafundisha watu wanaojitolea kukamata nyoka ili kuepusha watu kung'atwa kama ilivyo  pichani.
Thea Litschka-Koen
WHO hivi sasa inaelimisha wakazi wa Eswatini kuhusu nyoka na sumu zao na pia wanafundisha watu wanaojitolea kukamata nyoka ili kuepusha watu kung'atwa kama ilivyo pichani.

Watu 7400 hung’atwa na nyoka kila siku, WHO yachukua hatua

Afya

Je wajua kuwa watu 7400 hung’atwa na nyoka kila siku duniani kote na kati yao hao 220 hadi 380 hupoteza maisha?

Ni kwa kuzingatia kuwa ugonjwa utokanao na sumu ya nyoka ni miongoni mwa magonjwa ya kitropiki yaliyosahaulika, NTDs, ndio  maana shirika la afya ulimwenguni, WHO limetengeneza mkakati wa kupunguza kwa asilimia 50 matukio hayo ya nyoka kung’ata binadamu ifikapo mwaka 2030.

Mkakati dhidi ya nyoka

Mkakati huo ambao utazinduliwa baadaye mwezi huu wakati wa mkutano wa Baraza Kuu la WHO  unaangazia zaidi jinsi ya kujengea uwezo jamii ili iweze kupata tiba sahihi sambamba na mikakati ya kuimarisha mifumo ya afya ili huduma ya afya kwa wote ipatikane sambamba na kujenga ushirikiano baina ya wadau ndani ya nchi na baina ya kanda.

Miongoni mwa nchi ambazo wakazi wa vijijini wanaishi karibu zaidi na nyoka wenye sumu kali ni Eswatini ambako yakadiriwa kila mwaka kuna visa vya kati ya 200 hadi 400 vya watu kung’atwa na nyoka wenye sumu kali.

Aina ya nyoka kama kobra na songwe ndio tishio kubwa zaidi na sumu ya nyoka husababisha siyo tu kifo bali pia ulemavu wa viungo, upofu, kiwewe na hata watu kukatwa viungo vyao.

Nchini Eswatini zamani ikijulikana kama Swaziland, tayari hatua imechukuliwa ambapo mwakilishi wa WHO nchini humo Dkt. Cornelia Asyor ni miongoni mwa wataalamu walioshirikishwa kuchangia maandalizi ya mkakati huo utakaozinduliwa mwezi huu.

Nyoka aina ya Songwe akiwa ndani ya droo ya kabati. (Picha ya 2009)
Thea Litschka-Koen
Nyoka aina ya Songwe akiwa ndani ya droo ya kabati. (Picha ya 2009)

Hali ilivyo Eswatini

Katika maeneo ya vijijini nchini Eswatini, wananchi hukabiliwa na hatari ya kobra kuingia kwenye makazi yao.

Tayari taasisi ya Swaziland dhidi ya ung’twaji na nyoka, inaelimisha watu juu ya kuzuia uwezekano usio wa lazima wa kukutana na nyoka hao, kuondoa imani potofu kuhusu nyoka sambamba na kile ambacho wanapaswa kufanya iwapo wanang’atwa na nyoka.

Wakamata nyoka na waganga wa jadi

Pamoja na kuelimisha umma, taasisi hiyo pia inafundisha na kuweka orodha ya wakamata nyoka ambao wanajitolea kukamata nyoka hao ili kuepusha madhara kwa binadamu, halikadhalika kuelimisha umuhimu wa kuacha makazi asilia ya nyoka ili kuepusha mzozano kati ya nyoka na binadamu.

Hata hivyo WHO inasema imani za kijadi nazo zinakwamisha harakati za kukabiliana na nyoka. Ni kwa mantiki hiyo, “pindi mtu anapong’atwa na nyoka kimbilio la kwanza ni kwa mganga wa jadi.”

WHO inasema ni kwa kuzingatia hilo elimu pia kuhusu madhara ya sumu ya nyoka imeelezwa kwa waganga wa jadi ili hatimaye  waweze kuwaelekeza wagonjwa waende vitu vya afya.

Mkhulu ni manusura, yeye alikatwa mguu

Miongoni mwa manusura wa sumu ya nyoka ni Mkhulu (Pichani) ambaye alikuwa mkulima anayeheshimika sana huko Eswatini hadi pale alipong’atwa na nyoka aina ya Kobra na kubakia na ulemavu.

“Alipong’atwa na nyoka, hakukuwepo na dawa ya kukabili sumu hiyo na alisalia na kidonda kikubwa ambaho hakikupona na ililazimu akatwe mguu,” imesema WHO.

Taasisi ya Swaziland ilipokutana naye tayari alikuwa ni mlemavu aliyebakia tu kitandani akiwa na vidonda, umri wake ukiwa ni miaka 80. Tayari amepatiwa kitanda, kiti mwendo na taasisi inamsaidia kurejesha utu wake na pia kusaidia familia yake.