Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ukame watishia janga la kibinadamu Somalia- UN

Kaimu Naibu Mwakilishi Maalum wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa nchini Somalia, George Conway akiwa ziarani jimbo la Kusini-Magharibi nchini humo.
UN Photo.
Kaimu Naibu Mwakilishi Maalum wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa nchini Somalia, George Conway akiwa ziarani jimbo la Kusini-Magharibi nchini humo.

Ukame watishia janga la kibinadamu Somalia- UN

Tabianchi na mazingira

Umoja wa Mataifa umeonya kuwa hali ngumu itokanayo na ukame nchini Somalia inaweza kusababisha janga la kibinadamu iwapo hatua za dharura hazitachukuliwa kudhibiti hali hiyo.

Kaimu Naibu Mwakilishi Maalum wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa nchini Somalia, George Conway ametoa kauli hiyo baada ya kutembelea jimbo la Kusini-Magharibi na kujionea hali halisi ya kibinadamu wanayokabiliana nayo wananchi wakiwemo wakimbizi wa ndani.

Ziara yake ya siku moja akiambatana na maafisa kutoka Norwaya ilimpeleka kambi ya wakimbizi wa ndani ya Hawlwagaad huko Baidoa, ambako pamoja na kutembelea mradi wa shule kushuhudia harakati za shirika la kiraia kwenye eneo hilo za kuelimisha watoto ambao wamekimbia makwao kutokana na ukame, walikutana pia na wananchi waliokimbia makwao kutokana na ukame, na miongoni mwao ni Noorta Abdi Osman ambaye amesema,

(Sauti ya Noorta Abdi Osman)

“Tangu nifike hapa, shida zetu zimeongezeka. Kuna uhaba mkubwa wa maji. Hakukuwepo na elimu kwa watoto wetu, lakini angalau sasa kuna shule ya msingi Hawlwadaag inawafundisha watoto. Mahitaji yaw a wakimbizi wa ndani hapa kambini ni mengi tunahitaji msaada kutoka jamii ya kimataiaf na serikali ya jimbo la Kusini-Magharibi.”

Kwa mujibu wa ofisi ya Umoja wa Mataifa ya uratibu wa misaada ya kibinadamu, OCHA, hali ya ukame mwaka 2018/2019 na mvua zisizo za kutosha, imeongeza idadi ya watu wasio na uhakika wa chakula nchini Somalia ambapo Kaimu Naibu Mwakilishi Conway amesema,

(Sauti ya George Conway)

 “Changamoto kubwa sasa kwmaba ombi la usaidizi kwa mwaka 2019 limechangiwa kwa asilimia 19 tu hadi sasa na hii inatia wasiwasi kwa kuzingatia janga la kibinadamu linalonyemelea.”

Ujumbe huo ulikuwa na mazungumzo na Rais wa jimbo hilo la Kusini-Magharibi

Abdiaziz Hassan Mohamed  na wawakilishi wa mashirika ya kiraia na wakimbiz iwa ndani ambao baada ya kujadili janga la kibinadamu litokanalo na ukame amesema,

(Sauti ya Abdiaziz Hassan Mohamed)

 “Leo tumepokea ujumbe uliofika hapa kutathmini hali ya kibinadamu jimboni Kusini-Magharibi hususan Baidoa. Tumejadili changamoto zilizopo, hasa kuchelewa kwa mvua kunyesha na jinsi ya kuimarisha msaada wa kibinadamu na kusaka rasilimali kwa ajili ya watu walioathirika.”

Tayari Norway inasaidia miradi mjini Baidoa na inapanga kuongeza usaidizi wake wa kibinadamu jimboni Kusini-Magharibi kwa ushirikiano na Umoja wa Mataifa.

Mwaka jana, ukame ulisababisha watu milioni 6.2 nchini Somalia kuhitaji msaada wa dharura wa chakula, maji na malazi, hali ambayo ilisababisha Umoja wa Mataifa uzindue ombi la dola bilioni 1.6 kusaidia kushughulikia tatizo hilo.