Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

 Inawezekana kuishi pamoja kwa amani duniani:Moratino

Mandhari ya mji wa Baku nchini Azerbaijan
Picha: wiraza ya utalii na utamaduni ya Azerbaijan
Mandhari ya mji wa Baku nchini Azerbaijan

 Inawezekana kuishi pamoja kwa amani duniani:Moratino

Utamaduni na Elimu

Kuishi pamoja kwa amani ni jambo linalowezekana , lakini kurejea kwa kile kinachoitwa chuki, kunatia hofu kubwa ya utangamano. Kauli hiyo imetolewa na Miguel Angel Moratinos  ambaye ni mwakilishi wa Umoja wa Mataifa kwa ajili Muungano wa ustaarabu UNOAC  mjini Baku Azerbaijan ambako leo linaanza jukwaa la Umoja wa Mataifa kuhusu “majadiliano ya hatua dhidi ya ubaguzi, kutokuwepo kwa usawa na migogoro.”

Bwana Moratinos amesema jukwaa hilo la tano la kimataifa limekuja katika wakati muafaka kwani ”Chuki ni neno linalochagiza jamii kusambaratishwa, inawafanya watu kufikia hatua ya kutoweza kuishi pamoja katika mwelekeo wa kuwatokomeza wapinzani wao na hii ni hatari kubwa.”

Amesisitiza kuwa jukwaa hilo la muungano wa ustaarbbu ni muhimu kufikisha ujumbe mzito kwa jumuiya ya kimataifa kuwa “inawezekana kuishi pamoja na kwamba tunaweza kuheshimiana na tunapaswa kuelewa vyema tofauti za tamaduni na dini.”

Haji Gayib's moja ya majuka ya kihistoria mjini Baku nchini Azerbaijan lililojengwa katika karne ya 15
UN News/Elizabeth Scaffidi
Haji Gayib's moja ya majuka ya kihistoria mjini Baku nchini Azerbaijan lililojengwa katika karne ya 15

Moratinos amesema dunia inazidi kuingia katika hali ya sintofahamu na hivyo mkakati wa kimataifa kwa ajili ya majadiliano ya tamaduni mbalimbali ni ya muhimu sasa kuliko wakati mwingine wowote.

Ameongeza kuwa suluhu kupitia fedha, njia za kijeshi na njia za kisiasa inachukuwa mtazamo rahisi , lakini suluhu ya kudumu na endelevu “ inahitaji mtazamo wa kijamii na kitamaduni na ambao utachimba mizizi ya jamii mbalimbali ili kuweka hali halisi bayana. Hadi pale utakapoelewa mtazamo wa jirani yako, historia ya suala la chuki, jinsi gani umeingia katika mazingira hayo, yana athari gani na uhusiano uliopo, itakuwa vigumu sana kupata suluhu endelevu.”

Jukwaa hilo la kimataifa la siku mbili litakalokunja jamvi kesho Mei 3 linatathimini kwa kina jukumu muhimu la majadiliano ya tamaduni tofauti kama mkakati wa hatua kwa ajili ya ujenzi wa mshikamano na kuzisaidia jamii kukabiliana na machafuko na ubaguzi katika jamii mchanganyiko.

Kongamano hilo limewaleta pamoja washiriki zaidi ya 450 kutoka mashirika ya kimataifa, Umoja wa Mataifa, wawakilishi wa nchi , taasisi za kidini na asasi za kiraia.