Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Wakazi wa Gao warejea kujenga mji wao licha ya amani kusuasua

Harakati za kuinua kipato cha  jamii nchini Mali ambapo mkulima huyu kupitia mradi wa matokeo ya haraka wa MINUSMA amevuna bamia zake.
MINUSMA/Harandane Dick
Harakati za kuinua kipato cha jamii nchini Mali ambapo mkulima huyu kupitia mradi wa matokeo ya haraka wa MINUSMA amevuna bamia zake.

Wakazi wa Gao warejea kujenga mji wao licha ya amani kusuasua

Amani na Usalama

Nchini Mali, licha ya ukosefu wa amani ya kudumu kwenye mji wa kaskazini wa Gao, baadhi ya wananchi waliokimbia eneo hilo wameanza kurejea ili kusaidia ujenzi mpya na uponyaji kwa wale walioathiriwa na mzozo. 

Tupo katika hospitali ya rufaa iliyopo mjini Gao kaskazini mwa Mali, ambapo anaonekana Jamilla Amadou, muuguzi huyu, akipima kiwango cha shinikizo la damu cha mmoja wa wakazi wa eneo hili.

Jamila, ni mmoja wa waliorejea Gao baada ya kukimbia eneo hili mwaka 2012 wakati vikundi vya wapiganaji wenye msimamo mkali vilipotwaa mji huu. Sasa amerejea anatumia stadi zake za uuguzi kuleta matumaini na furaha kwa walio na magonjwa.

Kituo hiki kinatoa huduma za wajawazito kujifungua, watoto wachanga, watoto na pia kina kitengo cha kupiga picha za X-Ray ambapo Jamilla anasema,  “tunahudumia wagonjwa. Watu wanafika hapa na aina mbalimbali za matatizo kama vile kuhara, homa ya matumbo na shinikizo la damu. Tunahudumia zaidi watoto  kuliko watu wazima na hili ni jambo muhimu.”

Mlinda amani wa kikosi cha MINUSMA akiwa doria katika mitaa ya Gao, nchini Mali.
Marco Dormino
Mlinda amani wa kikosi cha MINUSMA akiwa doria katika mitaa ya Gao, nchini Mali.

Jamilla anasema tangu utotoni ndoto yake ilikuwa kuvaa koti jeupe na kuwa muuguzi lakini kitendo cha Gao kutwaliwa na vikundi vyenye msimamo mkali mwaka 2012 kilipeperusha ndoto yake kwani vifaa vya hospitali viliporwa.

Akikumbuka hali ilivyokuwa Jamilla anasema, “vitu viliporwa mwezi Aprili 2012. Kila kitu hatukuwa na milango, madirisha, hakuna kitu. Lakini hata sasa haiko kamilifu. Lakini ukilinganisha na mwaka 2012 na 2013, sasa ni bora.”

Maboresho hayo ni kazi ya shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi,  UNHCR na wabia wake ambao ni mashirika ya kiraia na wadau.

Mkataba wa amani na maridhiano nchini Mali wa mwaka 2015 bado unakosa uungwaji mkono na utekelezaji wake unasuasua.