Wataalam wa UN watoa wito serikali ya Ufilipino kusitisha mashambulizi dhidi ya Victoria Tauli-Corpuz

1 Mei 2019

Madai ya uongo yanayoelekezwa dhidi ya mtaalam maalum wa Umoja wa Mataifa kuhusu haki za watu wa asili na serikali ya nchi yake Ufilipino hayana mashiko kiukweli au kisheria na ni lazima yasitishwe haraka iwezekanavyo imesema taarifa ya wataalam wenzake iliyotolewa leo Jumatano na ofisi ya haki za binadamu ya Umoja wa Mataifa, OHCHR mjini Geneva, Uswisi

Katika taarifa ya pamoja, wataalam maalum wa Umoja wa Mataifa au wataalam huru wamesema, “madai mapya dhidi ya mtaalam mwenzetu, Victoria Tauli-Corpuz, yametolewa na viongozi serikalini ya rais Rodrigo Duterte, “kwa hakika kutokana na kazi yake adhimu anayaofanya kutetea haki za binadamu na watu wa asili kote ulimwenguni.”

Maafisa wa serikali wamedai kwamba Bi. Corpuz anashirikiana na chama cha kikomunisti kusini mashariki mwa visiwa vya Ufilipino na shughuli zao za kigaidi.

Mnamo Machi 13 mwaka huu , naibu mkuu wa operesheni za kijeshi Brigedia Generali Antonio Parlade, akihutubia waandishi habari mji mkuu Manila alidai kwamba Umoja wa Mataifa umeingiliwa na wanachama wa kikomunisiti wa Ufilipino kupitia Bi. Tauli-Corpuz.

Hali ii inakuja licha ya kwamba mahakama mjini Manila tarehe 27 mwezi Julai mwaka  jana ilitoa amri ya kutolewa kwa jina la mtaalam huyo kutoka kwenye orodha iliyofikishwa mbele ya mahakama na idara ya haki kutangaza chama hicho cha kikomunisit kama kundi la kigaidi.

Taarifa ya wataalam hao inasema kwamba Bi. Tauli-Corpuz mara kwa mara amelengwa na mamlaka na kudaiwa kuwa mwanachama wa kundi la kigaidi n mwanachama wa kundi la New People’s Army.

Aidha mwaka jana msemaji wa raisi Duterte alidai hadharani kwamba mtaalam huru huyo alilenga kuaibisha mamlaka.

“Madai ya uhalifu na mamlaka za Ufilipino zinadunisha kazi muhimu ya watetezi wa haki, inawaathiri mtazamo wao kwa jamii na huenda ikahatarisha maisha yao, au ukatili au mifumo mingine ya unyanyasaji,” wamesema wataalam.

Kwa mantiki hiyo wataalam hao wamesema, “tunatoa wito kwa serikali ya Ufilipino kusitisha mara moja mashambulizi yasiyokubalika dhidi ya kazi za haki za binadamu za Bi. Tali Corpuz na kuhakikisha usalama wake.”

Wataalam hao ambao wameongea kwa niaba yake ni mtaalam maalum wa Umoja wa Mataifa kuhusu watetezi wa haki za binadamu, Michel Forst, David Kaye anayehusika na uhuru wa kujieleza na Fionnuala Ní Aoláin anayehusika na kuchagiza  na kulinda haki za binadamu na haki za msingi za uhuru wakati wa kukabiliana na ugaidi.

 

 

♦ Kutembelea ukurasa maalum wa COP26 bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter