Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

ILO Afrika Mashariki yaungana na wenyeji kusherehekea siku ya wafanyakazi

Funguo tatu zikiwakilisha ushirikiano wa utatu wakati wa uzinduzi wa jengo la ILO tarehe 6 Juni mwaka 1926. Utatu huo ni serikali, biashara na wafanyakazi.
ILO
Funguo tatu zikiwakilisha ushirikiano wa utatu wakati wa uzinduzi wa jengo la ILO tarehe 6 Juni mwaka 1926. Utatu huo ni serikali, biashara na wafanyakazi.

ILO Afrika Mashariki yaungana na wenyeji kusherehekea siku ya wafanyakazi

Masuala ya UM

Leo ni siku ya wafanyakazi duniani, au Mei mosi ambapo mataifa ikiwemo yale ya barani Afrika yameadhimisha siku hiyo huku shirika la kazi ulimwenguni ukanda wa Afrika Mashariki likitoa wito kufanya kazi kwa pamoja kwa ajili ya kuchagiza usawa, haki kwa jamii na kuimarisha mazingira ya kazi kwa wote. 

ILO imekuwa mstari wa mbele katika kuchagiza mazingira bora ya kazi ikiwemo muda wa saa nane ambao mtu anahitaji kufanya kazi, likizo yenye malipo,siku ya mapumziko, likizo ya uzazi na kadhalika.

Maadhimisho ya siku ya wafanyakazi ni muhimu kwa kundi hilo ambalo linasongesha mbele uchumi wa nchi  kwa kuwa wafanyakazi hutarajia kusikia mabadiliko katika sekta ya ajira au hali ilivyo. 

Nchini Tanzania maadhimisho yamefanyika kitaifa mkoani Mbeya ambako mtaalam wa masuala ya ajira wa ILO Jealous Chirove akizungumza mjini Mbeya kwa niaba wa mkurugenzi wa ILO kanda ya Afrika,  amesema, “kuheshimiwa kazini, mishahara ya kutosha, saa nane za kazi  kwa siku na uhuru wa kujiunga na vyama. Kwenye katiba ya shirika la kazi duniani maneno ya awali yanasema amani ya kudumu ulimwenguni  inaweza kuwepo endapo kuna haki ya kijamii. Muundo wa ILO wa utatu ndio chanzo cha ushirikiano, wafanyakazi, waajiri na serikali kufanya kazi pamoja kwa kuwa na majadiliano ya karibu na kufikia mwafaka.”

Mgeni rasmi alikuwa Rais wa Tanzania John Magufuli ambaye amenukuu maudhui ya siku ya wafanyakazi duniani mwaka huu yanayogusia pia masuala ya mshahara ambapo amesema kuwa bado ahadi  yake aliyotoa mwaka jana wakati wa maadhimisho ya Mei Dei, iko pale pale ya kuongeza mshahara. "Ndugu zanguni bado sijaondoka madarakani na ahadi yangu ya nyongeza ya mshahara kwa wafanyakazi bado iko pale pale," amesema Rais Magufuli.

Maadhimisho ya mwaka huu yanafanyika wakati ILO ikitimiza miaka 100 tangu kuasisiwa hapo 1919.