Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Kongamano la kukabiliana na kauli za chuki yafungua pazia Geneva

Mjumbe maalum wa Umoja wa Mataifa kuhusu uzuiaji wa mauaji ya kimbari Adama Dieng.
UN Photo.
Mjumbe maalum wa Umoja wa Mataifa kuhusu uzuiaji wa mauaji ya kimbari Adama Dieng.

Kongamano la kukabiliana na kauli za chuki yafungua pazia Geneva

Haki za binadamu

Ofisi ya Umoja wa Mataifa mjini Geneva Uswisi imefanya kongamano kwa ajili ya kukabiliana na kauli za chuki ili kulinda vikundi vidogo vya kidini, wakimbizi na wahamiaji.

Kongamano hilo ambalo limeandaliwa kwa pamoja na mjumbe maalum wa Umoja wa Mataifa kuhusu uzuiaji wa mauaji ya kimbari Adama Dieng, linaendana na dhamira ya Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, António Guterres kukabiliana na misimamo mikali na kubuni mpango wa kuchukuahatua.

Kwa mujibu wa waandaji wa kongamano hilo la pili kuhusu dini, amani na usalama linafanyika wakati huu ambapo kuna ongezeko la uhasama kati ya mataifa na watu.

Akizungumza kwenye kongamano hilo bwana Dieng amesema, “Umoja wa Mataifa unachukua hatua za kukabiliana na hotuba za chuki ambazo zinadidimiza maadili ya pamoja na mambo ya msingi yanayokubalika kimataifa, katika Umoja wa Mataifa tunaamini kwamba kukaa kimya hakukubaliki na kukosa kuzungumza dhidi ya vitendo hivyo huenda kukaashiria kutokubali vinafanyika wakati hali ikiendelea kuwa mbaya na kugeuza walio hatarini kuwa wahanga.”

Ameongeza kuwa, “tunaamini kwamba juhudi katika kukabiliana na hotuba za chuki zitasaidia katika kusongesha mbele  hatua za vipaumbele katika ajenda ya Umoja wa Mataifa ikiwemo kuzuia mizozo, uhalifu na ukatili, kukabiliana na ukatili wa kijinsia na kuzuia aina nyingine za ukiukaji wa haki za binadamu na kuimarisha jamii zenye amani na zilizojumuishi n ani kiini cha ajenda ya maendeleo endelevu ya mwaka 2030.

Bwana Dieng amesema tayari ofisi yake imebuni mpango maalum wa kukabiliana na hotuba za chuki kufuatia pendekezo la Katibu Mkuu kuhusu mpango maalum utakaotumika na Umoja wa Mataifa.

Kwa upande wake Kamishna Mkuu wa haki za binadamu, Michelle Bachelet kupitia ujumbe wa video kwenye kongamano hilo amesema, “haki za bindamu zinauhusiano mkubwa na dini, usalamna na amani, viongozi wa kidini wana wajibu mkuwab katika kulinda haki za binadamu, amani na usalama au kwa bahati mbaya kudidimiza haki hizo kuunga mkono juhudi za washika dau wa dini ni muhimu kama ilivyo muhimu kulinda matumizi mbaya ya Imani za kidini kama silaha vitani na kutumiwa kuwanyima watu haki.”

Bi Bachelet ameongeza kuwa, “haki za binadamu na imani zinaweza kusaidia juhudi za pamoja, kwani watu wengi wa kidini wanafanya kazi katika kusongesha haki za binadamu kwa sababu ya misimamo waliyo nayo kuhusu kulinda haki za binadamu, usawa wa kijinsia na usawa, ninaamini kwamba viongozi wa dini wanaweza kuimrisha Imani na maelewano katika jamii.”

Naye mkurugenzi mkuu wa Umoja wa Mataifa Geneva, Michael Møller amesema hotuba za chuki zinaenea kama moto wa kichakani kupitia mitandao ya kijamii na vyombo vya habari. Aidha ameongeza kuwa“ni adui dhidi ya maadili yetu, usalamwa wa kijamii na kwa amani. Hotuba kama hizo za chuki zinazaa maovu mengi. Amesisitiza kuwa mashambulizi yaliyotokea New Zealanda na Sri Lanka yanaashiria dhana ya kwamba mtu mmoja si binadamu sawa na mwingine.”

Bwana Møller amasisitiza kwamba  wakati matukio kama hayo yakitokea ni muhimu kukumbuka kuwa watu wengi huonesha hisia za maelewano, ukarimu, haki na maridhiano.