Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Yemen acheni kuadhibu watu kwa misingi ya imani zao- Wataalamu

UN Photo/Martine Perret
Moja wa kizuizi
UN Photo/Martine Perret

Yemen acheni kuadhibu watu kwa misingi ya imani zao- Wataalamu

Haki za binadamu

Watalaam wa haki za binadamu wa Umoja wa Mataifa wametaka mamlaka zilizoko hivi sasa Yemen kutupilia mbali mara moja adhabu ya kifo aliyohukumiwa Hamid Kamali bin Haydara, kwasababu tu ya kuwa muumini wa dini ya Bahá’í.

Kupitia taarifa yao iliyotolewa leo mjini Geneva, Uswisi na ofisi ya haki za binadamu ya Umoja wa Mataifa, wataalamu hao wamesema, “hatuwezi kukubali ukosefu wa haki wa mtu kuhukumiwa kwa misingi ya imani yake au dini yake au tu kwa kuwa mfuasi wa dini ambayo ni ya kundi dogo.”

Wataalam hao wamesema hukumu kama hiyo sit u inakiuka kwa kiasi kikubwa haki za kimataifa za kibinadamu bali pia mahakama husika inaweza kuwa inatuma ujumbe usio sahihi kwa taifa zima la Yemen na ulimwenguni kote iwapo hukumu hiyo dhidi ya Haydara itatekelezwa.

Wamesema, “haki ya uhai na haki ya uhuru wa kuabudu au kuwa na dini ni haki ambazo serikali haziwezi kuzibadili kwa misingi yoyote ile na zinapaswa kuheshimiwa wakati wowote.”

Tarehe 2 mwezi Januari mwaka 2018, mahamaka mahsusi ya uhalifu nchini Yemen ilimhukumu Haydara adhabu hiyo kwa tuhuma za uhusiano na Israel na jamii za wayahudi na pia kueneza imani ya wabahai nchini Yemen.

Rufaa ya mwisho ya Haydara dhidi ya uamuzi huo ilisikilizwa tarehe 2 mwezi huu wa Aprili mjini Sana’a.

Wataalamu wamesema kuwa shtaka la kutishia uhuru wa Yemen halikidhi kigezo cha uhalifu wa kupindukia wa kuwezesha kuhukumu adhabu ya kifo kwa mujibu wa sheria za kimataifa.

“Si tu mwendesha mashtaka ameharamisha imani ya Bahá’í kwenye andiko lake bali pia ametishia waziwazi kuwa mtu yeyote ambaye atafanya kazi kumtetea Haydara atakuwa ni kibaraka.

Wametaka mamlaka zikishatupilia mbali hukumu hiyo zimwachie huru mara moja na ziache kutishia mawakili wanaomtetea.