Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Zaidi ya watoto 300,000 raia wa Venezuela walioko Colombia wanahitaji msaada wa kibinadamu: UNICEF

Tarehe 23 Aprili 2019 Cucuta Colombia (kulia) mkurugenzi wa UNICEF kitengo cha  mawasiliano Paloma Escudero akizungumza na wanawake na watoto kwenye kituo kinachosaidiwa na UNICEF
UNICEF/Santiago Arcos
Tarehe 23 Aprili 2019 Cucuta Colombia (kulia) mkurugenzi wa UNICEF kitengo cha mawasiliano Paloma Escudero akizungumza na wanawake na watoto kwenye kituo kinachosaidiwa na UNICEF

Zaidi ya watoto 300,000 raia wa Venezuela walioko Colombia wanahitaji msaada wa kibinadamu: UNICEF

Wahamiaji na Wakimbizi

Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto UNICEF limesema linasaka dola milioni 29 ili kuongeza bajeti yake ambayo kwa sasa ni takribani dola milioni sita tukwa lengo la kuwasaidia maelfu ya Watoto wa Venezuela wanaoishi nchini Colombia.

Kwa mujibu wa taarifa ya UNICEF iliyotolewa leo takriban watoto 327,000 kutoka Venezuela wanaishi kama wahamiaji na wakimbizi nchini Colombia , na bila ongezeko la msaada afya zao, elimu, ulinzi na mustakabali wao viko mashakani.

Taarifa hiyo inasema hali ya kisiasa nchini Venezuela imesababisha watu wapatao milioni 3.7 kufungasha virago nchini Venezuela na kukimbilia Brazil, Colombia, Ecuador, Peru na chi zingine katika kanda hiyo.

Miongoni mwa watu hao milioni 1.2 wako nchini Colombia na mara nyingi wanaishi katika jamii ambazo zinawahifadhi ambazo tayari ziko katika hali ngumu. Akizungumzia ukarimu wa Colombia mkurugenzi wa mawasiliano wa UNICEF ambaye amemaliza ziara ya siku nne kwenye jimbo la Cucuta upande wa Colombia mpakani mwa Venezuela, Paloma Escudero amesema “Katika wakati huu ambapo chuki dhidi ya wageni inaongezeka kote duniani , Colombia imekuwa mkarimu sana kwa kuacha milango yake wazi kwa jirani zake kutoka Venezuela.”

Ameongeza kuwa wakati “Familia nyingi zinafanya maamuzi magumu ya kuondoka makwao Venezuela kila siku , ni wakati kwa jumuiya ya kimataifa kuongeza juhudi za msaada ili kukidhi mahitaji ya msingi ya watu hao.Hatuwezi kuufanya ukarimu huo ukapotea bure.”

Waathirika

Katika daraja la Simon Bolivar linalounganisha Venezuela na Colombia , Escudero amezungumza na familia zinazofanya safari kila siku kutafuta huduma za afya, kupeleka Watoto wao shuleni, kutafuta chakula na kuleta mahitaji mengine ya msingi kwa ajili ya familia zao zilizosalia nyumbani.

“Nimekutana na mama mwenye kifafa na ana ujauzito wa miezi minane. Alihitaji kuja Colombia kupata vipimo vya ujauzito na kulinda afya ya mtoto wake. Kwa familia nyingi uamuzi wa kuondoka ni changuo la mwisho kabisa. Hali mbaya nchini Venezuela iimewaacha wazazi wengi bila chaguo lolote bali kusaka fursa za elimu kwa ajili ya watoto wao upande wa pili wa mpaka.”

Colombia inatoa elimu ya bure kwa watoto wahamiaji kutoka Venezuela . Zaidi ya watoto 130,000 kutoka Venezuela wameandikishwa katika shule mbalimbali nchini Colombia ikiwa ni ongezeko kubwa kutoka 30,000 mwezi Novemba mwaka jana.

UNICEF inashirikiana kwa karibu na mashirika ya misaada ya kibinadamu , ya kitaifa na ya kijamii, mashirika yasiyo ya kiserikali na jamii za Colombia ili ili kuwapa huduma muhimu watoto wahamiaji wa Venezuela lakini pia wa kutoka jamii zinazowahifadhi , ikiwemo msaada wa afya, lishe, elimu, na ulinzi.

Lengo kwa mwaka huu

Hatua zilizochukuliwa hadi sasa ni pamoja na kusaidia timu za wahudumu wa afya, kuweka maeneo rafiki kwa ajili ya watoto kupata msaada wa kisaikolojia na kuzuia ghasia, kuwapa maji safi ya kunywa na masuala ya usafi, kutenga maeneo ya kujifunza, kuwagawia vifaa vya shule, kutoa mafunzo kwa waalimu na kutoa msaada wa lishe.

Pamoja na hayo yote UNICEF imesema kwa mwaka huu inalenga kusaidia kuwapa chanjo watoto zaidi ya 30,000, kutoa huduma ya maji na usafi mashuleni kwa watoto 130,000, kuwapa watoto 40,000 fursa ya elimu rasmi na isiyo rasmi, kuwafikia kina mama wanaonyonyesha 15, 000 na kuwapa huduma za lishe, na kuwafikia watoto na barubaru 90,000 kwa hatua za kuzuia na kushughulikia ghasia, ukatili na unyanyasaji ukiwemo wa kijinsia na pia kuzuia watoto kuingizwa katika masuala ya vita.