Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ubia wa UNHCR na EAA waleta nuru kwa watoto wakimbizi

Shule ya Fugee ambayo ilianzishwa 2009, imetoa elimu kwa takriban wakimbizi watoto 300.
Grace Tan / Payong
Shule ya Fugee ambayo ilianzishwa 2009, imetoa elimu kwa takriban wakimbizi watoto 300.

Ubia wa UNHCR na EAA waleta nuru kwa watoto wakimbizi

Wahamiaji na Wakimbizi

Kamishna Mkuu wa shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi, UNHCR Filippo Grandin a muasisi wa taasisi ya Elimu kuzidi vyote, EAA Sheikha Moza bint Nasser wa Qatar, wako nchini Malaysia ambako wameshuhudia jinsi EAA iliyosaidia kuelimisha watoto wakimbizi wa ndani na wale waliotoka nchi jirani.

Wawili hao wameshuhudia mafanikio ya mradi mmoja kati ya miradi 131 ambayo UNHCR na EAA inatekeleza kwa lengo la kuandikisha shuleni watoto wakimbizi 450,000 katika mataifa 15 kote duniani.

Malaysia ambayo ni taifa lenye wakimbizi 167,000. EAA na wadau wake wamesaidia zaidi ya watoto wakimbizi 9,400 kutoka zaidi ya mtaifa 17 kwenda shuleni.

Akizungumza kwenye kituo hicho cha Dignity, Shekha Moza ambaye pia ni mchechemuzi wa wa malengo endelevu ya Umoja wa Mataifa, SDGs, amesema “ni dhahiri kuwa kwa kile tunachoshuhudia hapa Malaysia kuwa elimu bora ya msingi inaweza kubadilisha mwelekeo wa maisha ya mtoto.”

Amesema kuwapatia wakimbizi ufahamu na stadi kunamaanisha kuwa wanaweza kuwa rasilimali bora kwa nchi inayowahifadhi na pia baadaye kujenga nchi zao pindi wanaporejea nyumbani.

“Ninajivunia sana kwa kazi inayofanyika hapa na nashukuru Malaysia na watu wake kwa kusaidia watoto hawa kuwa na mustakabali bora,” amesema mchechemuzi huyo wa SDGs.

Kwa upande wake, Kamishna Mkuu wa UNHCR amesema kuwa, “siweze kusisitiza zaidi umuhimu wa maeneo sahihi ya shule kwa ajili  ya watoto wakimbizi wa nje na wale wa ndani ambao mamilioni kati yao wanapoteza fursa ya shule kila mwaka.”

Amesema kuwapatia elimu bora sit u kunasaidia watoto kupona makovu bali pia kunaleta utulivu kwenye familia zao, na kufanya wakubalike katika jamii na kuwa na matumaini ya baadaye.

Hivi sasa, kuna wakimbizi milioni 68.5 kote duniani ambapo zaidi ya milioni 25 ni wakimbizi ugenini ilhali milioni 40 ni wakimbizi ndani ya nchi zao.

Ubia kati ya UNHCR na EAA utawezesha kuwepo kwa mchango wa pamoja wa dola milioni 100 kusaidia mafunzo kwa watoto wakimbizi wa kutoka nje na wale wa ndani.

Hadi sasa EAA na wadau wake wanasidia zaidi ya watoto milioni 7.5 wasio shuleni katika mataifa 50 ambapo kati yao hao milioni 2.3 ni watoto wakimbizi.