Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Teknolojia ya fedha kiganjani yasaidia wanawake kujiimarisha kibiashara huku wakitunza familia zao -Benki Kuu ya Kenya

Patrick Njoroge, Gavana wa benki kuu ya Kenya katika jukwaa la shirika la fedha duniani kujadili mustakabali wa pesa na malipo katika karne ya kidjitali katika makao makuu ya IMF.
IMF Staff Photograph/Stephen Jaffe
Patrick Njoroge, Gavana wa benki kuu ya Kenya katika jukwaa la shirika la fedha duniani kujadili mustakabali wa pesa na malipo katika karne ya kidjitali katika makao makuu ya IMF.

Teknolojia ya fedha kiganjani yasaidia wanawake kujiimarisha kibiashara huku wakitunza familia zao -Benki Kuu ya Kenya

Ukuaji wa Kiuchumi

Maendeleo ya kidijitali yanabadilisha shughuli za kiuchumi duniani na kudidimiza matumizi ya pesa taslimu huku ikibua mifumo mipya ya pesa na malipo.          

Gavana wa Benki Kuu ya Kenya Patrick Njoroge amesema hayo hivi karibu wakati wa jukwaa la shirika la fedha duniani, IMF lililojumuisha wawakilishi kutoka Benki Kuu za mataifa mbali mbali na sekta binafsi wakijaili kuhusu mustakabali wa pesa na malipo na nafasi ya sekta binafsi na benki kuu za nchi.

Bwana Njoroge amesema mifumo ya kidijitali imebadili uendeshaji biashara akitoa mfano wa utafiti nchini Kenya

(Sauti ya Patrick Njoroge)

“Tulikuwa tunaangalia taarifa katika moja ya jukwaa letu la kutoa mikopo na tuligundua kwamba idadi kubwa ya miamala inafanyika kati ya saa tisa hadi saa 11 alfajiri. Tulichunguza na kugundua takriban asilimia 40 ya washiriki ni wanawake, na hivyo likaiubuka suala iweje, wanawake hawalali ? »

Hata hivyo uchunguzi ulibaini kwamba

(Sauti ya Patrick Njoroge)

«Cha msingi kuna wafanyabiashara katika soko na wananunua bidhaa ambazo wanaziuza barabarani na kwenye vibanda kwa hiyo wanapoamka saa tisa alfajiri wanatumia simu zao kukopa mkopo katika jukwaa kisha watapiga simu kwa muuza bidhaa za jumla kununua gunia la bidhaa fulani na kulipa kwa njia ya simu, kisha wapigie simu msafirishaji bidhaa na kumuagiza azipeleke kwenye kibanda chake. Na hapo mwanamke huyo ataendelea na majukumu ya kuwaanda watoto na saa 11 alfajiri atakuwa kwenye kibanda chake na bidhaa tayari kufanya biashara.”

Bwana Njoroge ameongeza kwamba jukwaa kama hilo sio tu lina faida za kiuchumi lakini pia kijamii.

Kwa mujibu wa tafiti, hivi sasa upenyo wa simu za mkononi ni asilimia 105.