Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Uganda na uungaji mkono wa juhudi za UN za kuleta amani Somalia

Askari wa kike kutoka Uganda anayehudumu kwenye kikosi cha ulinzi cha Umoja wa Mataifa,  UNGU nchin Somalia akiwa na kitazama mbali wakati akiwa lindoni kwenye mji mkuu wa Somalia, Mogadishu
UN /Ilyas Ahmed
Askari wa kike kutoka Uganda anayehudumu kwenye kikosi cha ulinzi cha Umoja wa Mataifa, UNGU nchin Somalia akiwa na kitazama mbali wakati akiwa lindoni kwenye mji mkuu wa Somalia, Mogadishu

Uganda na uungaji mkono wa juhudi za UN za kuleta amani Somalia

Amani na Usalama

Kikosi cha walinda amani 530 kutoka Uganda kipo nchini Somalia kwa ajili ya kusaidia kuleta amani na utulivu. Kikijumusha wanawake 63 na wanaume 467, kikosi hicho ni sehemu ya kikosi cha ulinzi cha Umoja wa Mataifa, UNGU, ambacho jukumu lake ni kulinda maeneo ya Umoja wa Mataifa kwenye mji mkuu Mogadishu ili kusaidia ujumbe wa umoja huo nchini Somalia, UNSOM na ofisi ya usaidizi wa Somalia, UNSOS ziweze kutekeleza mamlaka zao.

Kazi yao inakabiliwa na hatari kubwa. Shambulio kwenye eneo la ofisi za Umoja wa Mataifa mwezi Januri mwaka huu, “bado liko kwenye fikra zao,” amenukuliwa kamanda wa walinda amani kutoka Uganda ambao walikuwa na jukumu la kulinda eneo hilo.

Siku ya mwaka mpya, makombora saba yalitua ndani  ya eneo hilo, lililoko mji mkuu wa Somalia, Mogadishu na kujeruhiwa wafanyakazi wawili wa Umoja wa Mataifa na mkandarasi mmoja. Kundi la kigaidi la Al-Shabaab liliripotiwa kukiri kuhusika na shambulio hilo.

“Hili lilikuwa shambulio lisilo la moja kwa moja kwenye eneo la Umoja wa Mataifa ndani ya kiwanja cha ndege cha kimataifa cha Mogadishu,” amesema Kanali Stuart R. Agaba, kamanda wa UNGU.

Kamanda wa kikosi cha ulinzi cha Umoja wa Mataifa nchini Somalia, UNGU, Kanali Stuart Agaba akizungumza wakati wa mahojiano mjini Mogadishu, Somalia
UN /Ilyas Ahmed
Kamanda wa kikosi cha ulinzi cha Umoja wa Mataifa nchini Somalia, UNGU, Kanali Stuart Agaba akizungumza wakati wa mahojiano mjini Mogadishu, Somalia

Hata hivyo kikosi hicho cha UNGU kilichukua hatua haraka kwa kujibu mashambulizi na kilikuwa tayari kusambaratisha shambulio lolote ambalo lingalifuatia.

Hii inajumuisha kuzuia na kulinda wafanyakazi na miundombinu ya Umoja wa Mataifa dhidi ya mashambulio yoyote na kufanya doria ndani ya eneo na kwenye viunga vyake. Walinda amani kutoka Uganda pia wamefundishwa kuwaondoa na kuwahamisha harakaka wafanyakazi wa Umoja wa Mataifa.

Hatari kubwa

Umoja wa Mataifa unaelezea hali ya Somalia kuwa ni ‘tete’ na hivi karibuni mjini Mogadishu kumekuwepo na ongezeko la kushamiri kwa vikundi vya kigaidi. Kwa mujibu wa Kanali Agaba, walinda amani wa Umoja wa Mataifa wanafanya kazi katika mazingira hatari ambayo ni kati ya kiwango cha kati na juu sana. 

Askari wanawake, kuanzia cheo cha juu hadi chini ni muhimu sana ndani ya UNGU kwa kuwa wanawapatia matumaini wanawake na watoto wa taifa hili,  Kanali Agaba, UNGU

Jeshi la wananchi wa Uganda, UPDF limekuwa likichangia walinda amani tangu mwaka 2015 na huu ni mzunguko wa tano ambao walinda amani hao wanahudumu kwenye UNGU.

Huu ni “uzoefu mpya kwa askari wanawake na wanaume kutoka UPDF,” ameseka Kanali Agaba akiongeza kuwa. “wana uzoefu mkubwa, wamejifunza ustahimilifu na jinsi ya kukabiliana na shinikizo na wanaelewa jinsi Umoja wa Mataifa unavyofanya kazi.”

Wanawake

Askari mwanamke kutoka Uganda anayehudumu kikosi cha ulinzi cha Umoja wa Mataifa, UNGU nchini Somalia akikagua gari kwenye kizuizi mjini Mogadishu
UN /Ilyas Ahmed
Askari mwanamke kutoka Uganda anayehudumu kikosi cha ulinzi cha Umoja wa Mataifa, UNGU nchini Somalia akikagua gari kwenye kizuizi mjini Mogadishu

Kwa sasa, kuna wanawake 63 wanaohudumu kwenye kikosi hicho cha UNGU. “Askari wanawake, kuanzia cheo cha juu hadi chini ni muhimu sana ndani ya UNGU kwa kuwa wanawapatia matumaini wanawake na watoto wa taifa hili,”Kanali Agaba, UNGU

Maafisa wanawake wanapelekwa kwenye ulinzi wa amani wakiwa na majukumu mbalibali kuanzia kusimamia vikosi, kusimamia usakaji na usalama pamoja na majukumu mengine ya ulinzi na pia wana dhima muhimu katika kituo cha operesheni za taarifa za kiusalama, SIOC.

Itikadi ya uwanamajumui

Somalia kwa Afrika Mashariki ni jirani wa karibu wa Uganda na kwa mujibu wa Kanali Agaba, mchango wa nchi yake kwenye ulinzi wa amani unatokana na itikadi ya uwanamajumui ambayo kwayo Uganda imeendelea kutumia ili kujitolea kwa ajili ya amani, ustawi na utulivu wa Somalia.

Na kama kamanda Kanali Agaba anavyoamini kwamba, “kwa kuhakikisha maafisa wa UNGU, wanawake kwa wanaume wanafanya kazi yao kwa ufanisi na kwa kuzingatia misingi ya Umoja wa Mataifa, hii inafanya mchango wetu kwenye juhudi za Umoja wa Mataifa kuleta amani duniani kuwa ni uzoefu wa kutosheleza.