Kasi ya Kenneth Msumbiji yapungua, UN yajipanga kusaidia waathirika

26 Aprili 2019

Baada ya kimbunga Kenneth kupiga jimbo la Cabo Delgado kaskazini mwa Msumbiji jana jioni, na sasa kuwa kimepungua kasi yake, Umoja wa Mataifa umechukua hatua ya kupeleka timu yake ili kusaidiana na serikali katika operesheni za usaidizi na usimamizi wa taarifa.

Kimbunga Kenneth ni kimbunga cha pili kupiga Msumbiji ndani ya msimu mmoja ambapo mwezi uliopita, eneo la kati mwa nchi hiyo lilikumbwa na kimbunga Idai kilicholeta madhara kwa binadamu, mali na miundombinu.

Tathmini ya awali ya shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto, UNICEF inaonyesha kuwa kimbunga Kenneth kimeathiri watu 16,776 , ambapo nyumba 2,934 zimebomoka kidogo, ilhali 450 zimeharibiwa kabisa, madarasa 31 yameharibiwa pamoja na vituo vitatu vya afya . UNICEF imesema nguzo 54 za umeme nazo zimenguka.

Shirika la hali  ya hewa duniani, WMO kupitia msemaji wake Claire Nullis linasema  hata hivyo madhara ya kimbunga Kenneth yalikuwa ni madogo kwa kuwa kilipunguza kasi kabla ya  kufika ardhini na kilitua eneo la mashambani na kwamba,  “mamlaka za Msumbiji zilihamisha maelfu ya watu hatua ambayo ilipunguza madhara ya vifo. Na Tanzania, ambayo haijawahi kukumbwa na kimbunga cha kitropiki, ilitoa matangazo ya hadhari mapema kwa watu walio hatarini na maonyo hayo yanaendelea hadi leo hii, maonyo ya mafuriko na maporomoko ya udongo.”

Madhara yaliyoripotiwa ni pamoja na mapaa ya nyumba kuezuliwa na mvua kubwa inayotarajiwa katika siku 10 zijazo, ikiwa ya kiwango cha mara mbili zaidi ya kile ambacho eneo la Beira lilipata wakati wa kimbunga Idai mwezi uliopita.

Msemaji wa ofisi ya Umoja wa Mataifa ya usaidizi wa dharura, OCHA, Jens Laerke amemnukuu mkuu wa ofisi hiyo Mark Lowcock, akielezea masikitiko yake na kwamba leo wametuma ujumbe wa nyongeza huko Pemba mji mkuu wa jimbo la Cabo Delgado kwa kuwa, “hatua baada ya kimbunga Kenneth zinaweza kuhitaji operesheni kubwa ya kibinadamu wakati huu ambapo operesheni za kusaidia waathirika wa kimbunga Idai kwenye nchi tatu bado hazijapata ufadhili wa kutosha. Familia ambazo maisha yao yamesambaratishwa na majanga haya yahusianayo na mabadiliko ya tabianchi yanahitaji ukarimu wa  jamii ya kimataifa ili ziweze kuhimili maisha miezi ijayo.”

Nalo shirika la mpango wa chakula duniani, WFP limesema linashirikana na serikali kuweza kusaidia watu 700,000 walio hatarini kuathiriwa na kimbunga hicho na tayari wamepeleka tani 500 za chakula huko Pemba, huku tani  nyingine 1,000 zikitarajiwa punde.

Hali baada ya kimbunga Kenneth kupiga eneo la Pemba nchini Msumbiji jana tarehe 25 Aprili 2019
WFP/Maktaba ya Picha
Hali baada ya kimbunga Kenneth kupiga eneo la Pemba nchini Msumbiji jana tarehe 25 Aprili 2019

Kwa mujibu wa WMO, utabiri wa hali ya hewa unaonesha kuwa mvua kubwa itaendelea kunyesha kwa siku kadhaa hata baada ya kutulia kwa pepo zitokanazo na kibmunga Kenneth na hiyo inaweza kusababisha mafuriko.

Kimbunga Kenneth kimepiga Msumbiji kwenye mkesha ambao WMO ilikuwa inapeleka jopo lake nchini humo kujadili na mamlaka kile ambacho imejifunza kutokana na kimbunga Idai na hatua zinazopaswa kuchukuliwa siku za usoni kupunguza madhara yatokanayo na majanga.

 

 

 

♦ Kurambaza ukurasa mahsusi wa Siku ya Kiswahili Duniani bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter