Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Uimarishaji amani Sahel uende sambamba na misaada ya kimkakati- FAO

Ukosefu wa usalama na ukame vimesababisha njaa ukanda wa Sahel na kulazima mashirika ya Umoja wa Mataifa kama WFP kulazimika kugawa mlo kwa wakazi wa eneo hilo.
WFP/Sébastien Rieussec
Ukosefu wa usalama na ukame vimesababisha njaa ukanda wa Sahel na kulazima mashirika ya Umoja wa Mataifa kama WFP kulazimika kugawa mlo kwa wakazi wa eneo hilo.

Uimarishaji amani Sahel uende sambamba na misaada ya kimkakati- FAO

Msaada wa Kibinadamu

Mkurugenzi Mkuu wa shirika la chakula na kilimo duniani, FAO José Graziano Da Silva aliyeko ziarani  nchini Senegal, amesema harakati zote za kusaka amani ya kudumu kwenye eneo la Sahel lazima ziende sambamba na uwekezaji mkubwa katika maendeleo vijiijni na kilimo.

Kauli  yake inazingatia ukweli kwamba, “mizozo, ukosefu wa chakula, utapiamlo, majanga ya asili na ukimbizi wa ndani pamoja na magonjwa vimeshamiri kwenye ukanda wa Sahel” amesema da Silva akiongeza kuwa iwapo hakuna hatua mujarabu kukabiliana na hali hiyo, wakazi wa eneo hilo wataendelea kuhitaji misaada ya dharura kila mwaka.

Kwa mujibu wa kamati ya kudumu ya kudhibiti ukame Sahel, watu milioni 6 kwenye ukanda huo walikabiliwa na njaa mwaka jana ambapo nusu yao ni wafugaji na wakulima wanaohusika pia na mifugo.

Bwana da Silva amegusia mpango wa pamoja wa FAO na Muungano wa Ulaya, EU wa kuimarisha uwezo wa watu kuwa na uhakika wa chakula sambamba na mnepo wakati wa msimu wa mwambo.

Mfumo huo wa pamoja wenye gharama ya Euro milioni 9 unalenga kusaidia watu 140,000 wengi wao wakiwa ni wafugaji walio hatarini zaidi kwenye ukanda wa jangwa wa Sahel.

Kupitia mradi huo, mtandao wa taarifa utasaidia watunga sera na wakulima wafugaji kwenye hatua zao za kuchagua kile ambacho wanataka kufanya na pia kuboresha mbinu za kilimo na ufugaji.

Mradi pia utaanzisha mashamba darasa 300 sambamba na kuendeleza utumiaji endelevu na shirikishi wa rasilimali asilia pamoja na biashara ya kuvuka mpaka.

Matarajio kwa mujibu wa FAO,  ni wakulima wafugaji kuwa na mbinu za kisasa, ardhi kuboreshwa na pia kuwepo kwa mbinu bora za uzalishaji wa majani ya lishe kwa mifugo.