Wanawake 8 kati ya 10 wanaofika kituo cha saratani Uganda wana saratani ya shingo ya kizazi

25 Aprili 2019

Shirika la afya duniani WHO limesema kimataifa eneo la Afrika Mashariki linabeba mzigo mkubwa wa saratani ya shingo ya uzazi huku Uganda ikiwa miongoni mwa nchi tano barani humo zenye wagonjwa wengi. 

Akizungumza kwenye kongamano kuhusu kupanua wigo wa chanjo dhidi ya virusi vinavyosababisha saratani ya shingo ya uzazi HPV mjini Kampala nchini Uganda hii leo  , mwakilishi wa masuala ya chanjo wa WHO

Dkt. Annet Kisake amesema Uganda ni miongoni mwa nchi tano zenye kiwango kikubwa cha wanawake wenye saratani ya shingo ya uzazi barani Afrika ambapo wanawake 8 kati ya 10 wanaofika na kufanyiwa uchunguzi kwenye taasisi ya saratani nchini Uganda wanaugua saratani ya shingo ya uzazi.

Dkt. Kisake ametaja baadhi ya vitu vinavyoweza kuepukwa ili kuwaeprsha wanawake wengi na saratani ya shingo ya uzazi nchini humo ikiwemo ndoa za utotoni, kuwa na wapenzi wengi wa kushiriki nao ngono, magonjwa ya zinaa ikiwemo HIV, matumizi ya bidhaa za tumbaku, ukosefu wa vitamina  na maambukizi ya virusi vya HPV.

Hata hivyo amesema serikali ya Uganda imechukua hatua kukabiliana na kuongezeka kwa ugonjwa huo ikiwemo kuanzisha chanjo ya HPV mwezi Novemba mwaka 2015 ambayo ilipangwa kutolewa katika wilaya zote nchini humo.

Ameongeza kuwa pamoja na jitihada hizo bado dozi ya pili ya HPV iko chini sana miaka mitatu tangu kuanza kwa chanjo hiyo Uganda.

Lakini sasa serikali serikali ya Uganda imeamua kuchukua mtazamo mpya wa kushirikisha seta mbalimbali katika vita hivi na wizara ya afya ikiwa ndio kiongozi kupitia mpango wa kitaifa wa chanjo UNEPI, wamejumuisha pia wizaya ya elimu na wizara ya michezo ikisema wakifanya kazi pamoja hatua zitafanikiwa zaidi na hususani kupanua wigo wa chanjo hiyo.

Akizungumzia hatua hiyo katika kongamano hilo waziri wa afya Sarah Opendi amesema mshimano unahitajika kutoka kwa wadau wote na wizara za elimu na michezo zitasaidia sana hasa katika kuhamasisha jamii na shule  ili kuhakikisha wanafunzi wanapata chanjo ya HPV. Pia amesema elimu hiyo itasaidia hasa kwa changamoto ya dhana iliyopo kwa baadhi ya jamii kuwa chanjo hiyo ina madhara.

Kongamano hilo lililomalizika leo limeandaliwa na Uganda kwa ushirikiano na WHO.

 

 

 

Shiriki kwenye Dodoso UN News 2021:  Bofya hapa Utatumia dakika 4 tu kukamilisha dodoso hili.

♦ Na iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter