UN yachukua hatua Msumbiji kukabili madhara ya kimbunga Kenneth

25 Aprili 2019

Kimbunga Kenneth kikitarajiwa kupiga maeneo ya kaskazini mwa Msumbiji jioni ya leo siku ya Alhamisi, Umoja wa Mataifa nchini humo umesema tayari umeanza kuchukua hatua ili kupunguza madhara ya kimbunga hicho ambacho pia kinatarajiwa kupiga maeneo ya kusini mwa Tanzania.

Mratibu wa masuala ya kibinadamu wa Umoja wa Mataifa nchini Msumbiji Marcoluigi Corsi, ameiambia Idhaa ya Umoja wa Mataifa kuwa, “kile ambacho tumefanya hadi sasa kama UN ni kuhamasisha timu yetu  kwenye mji mkuu wa jimbo la Cabolgado, Pemba ambayo inafanya kazi kwa ushirikiano na mamlaka za mitaa na kitaifa na tumeweka vifaa vya misaada vitakavyotumika kusaidia wilaya zitakazoathirika.”

Mapema Filipe Lucio kutoka mradi wa huduma za tabianchi WMO amesema ni vyema kuchukua hatua za dharura kwa kuwa kimbunga hicho kitaambatana na upepo wenye kasi ya kati ya kilometa 130 kwa saa hadi kilometa 180 kwa saa huku kiwango cha mvua kikitarajiwa kuwa kati ya meta 2 hadi 4 kutoka usawa wa ardhi.

Huku mamlaka hizo zikichukua hadhari, Bwana Lucio amesema, “ni kuelimisha umma kuhusu madhara ambayo kimbunga Kenneth kinaweza kusababisha. Lakini pia  hatua za kuchukua kama vile  kwenye miundombinu na makazi mbadala kwa watu ambao nyumba zao si imara. Upepo wa kasi ya kilometa 180 kwa saa unaweza kuzibomoa, kwa hiyo mawasiliano hayo lazima yafanyike kwa watu walio hatarini ili waweze kuchuka hatua.”

Bwana Lucio amesihi wakazi wa maeneo hayo wasichelee kuchukua hatua kwa kuwa kimbunga kinakuja na hatua zianze sasa ili wawe tayari pindi kimbunga kitakapopiga.

Mwezi  uliopita kimbunga Idai kilipiga majimbo manne ya Msumbiji na kusababisha madhara makubwa ya uhai wa  binadamu, mali na miundombinu.

 

♦ Tafadhali iwapo unataka kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud

Fuatilia Habari: Habari zilizopita za Mada Hii

Watoto ni waathirika wakubwa mwezi mmoja tangu kimbunga Idai-UNICEF

Mwezi moja tangu kimbunga Idai kukumba nchi za Msumbiji, Malawi na Zimbabwe, Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto, UNICEF, limetoa ombi la dola milioni 1.6 kusaidia watoto ambao wanaibuka kutoka athari zake mwezi mmoja tangu kimbunga hicho.

Vifo vya IDAI vinaongezeka , huku mlipuko kipindupindu waongeza hofu Msumbiji:OCHA

Kwa mujibu wa shirika la Umoja wa Mataifa la kuratibu masuala ya kibinadamu na misaada ya dharura OCHA , idadi ya vifo vilivivyosababishwa na athari za kimbunga Idai nchini Msumbiji imeongezeka na kufikia 493.