Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Nchini Mali chanjo zatolewa kwenye mikusanyiko ili kufikia kila mtoto

Mshauri wa mashinani kutoka UNICEF huko jimboni Kayes nchini Mali  akimweleza mama umuhimu wa kumpatia chanjo mwanae. (Machi 2019)
UNICEF/Seyba Keïta
Mshauri wa mashinani kutoka UNICEF huko jimboni Kayes nchini Mali akimweleza mama umuhimu wa kumpatia chanjo mwanae. (Machi 2019)

Nchini Mali chanjo zatolewa kwenye mikusanyiko ili kufikia kila mtoto

Afya

Ikiwa leo ni mwanzo wa wiki ya chanjo duniani, nchini Mali serikali kwa kushirikiana na wadau wameanzisha mbinu mpya za kuhakikisha kila mtoto anayetakiwa kupatiwa chanjo anapatiwa kama nija mojawapo ya kuepusha vifo vya watoto nchini humo. 

Mali nchi ambayo idadi kubwa ya magonjwa yanayoua watoto yanazuilika, watoto wanaopata chanjo ni asilimia 45 pekee ilhali asilimia 14 hawapati kabisa chanjo.

Ingawa serikali ya Mali na wadau wake wamepatia kipaumbele suala la chanjo, mtoto mmoja kati ya 10 nchini humo hufariki dunia kabla ya kufikisha  umri wa miaka mitano.

Hali ni mbaya sana katika jimbo la Kayes ambako jamii nyingi zinaishi kwenye maeneo yasiyofikiwa kwa urahisi na hivyo milipuko ya ugonjwa wa Surua hutokea mara kwa mara.

Eneo hili lina machimbo ya madini ambapo familia nyingi zinaishi na kusaka kipato huku watoto wao wakikosa huduma za afya ikiwemo chanjo.

Hata hivyo serikali imeibuka na mbinu mpya ya utoaji chanjo kwenye mikusanyiko ya watu iwe sokoni, shuleni, misikitini au vituo vikuu vya mabasi ambapo wahudumu wa afya husafiri kwa pikipiki au magari kutoa chanjo hizo.

Mama na mwanae katika kijiji cha Kombaka kilichoko  ndani zaidi nchini Mali akipatiwa kadi ya chanjo baada ya mwanae kupatiwa chanjo na mtumishi huy wa afya ataembea mguu kwa mguu kugawa chanjo
UNICEF/Seyba Keïta
Mama na mwanae katika kijiji cha Kombaka kilichoko ndani zaidi nchini Mali akipatiwa kadi ya chanjo baada ya mwanae kupatiwa chanjo na mtumishi huy wa afya ataembea mguu kwa mguu kugawa chanjo

Miongoni mwao ni Adama Traore ambaye husafiri kilometa 50 kutoka kituo cha afya ili kupatia chanjo wakazi wa maeneo ya migodini.

Fatoumata Tounkara ambaye watoto wake wanne waliugua surua ni mmoja wa wanufaika ambaye anasema kwamba, “ugonjwa ulianza na mwanangu Aboubacar Bah. Tulimpeleka hospitali walimpatia dawa na chanjo na tukarejea nyumbani. Tangu wakati huo alianza kujisikia vizuri. Lakini baada ya hapo aliambukiza nduguze. Ushauri wangu kwa wazazi wapatie chanjo watoto wao bila kuchelewa. Watoto wangu baada ya kutibiwa wote walipatiwa chanjo. Namshukuru Mungu hivi sasa hawajambo. Sasa naona umuhimu wa chanjo.”

Mpango wa chanjo nchini Mali unafanikishwa kwa ushirikiano baina ya serikali, shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto, UNICEF pamoja na fuko la chanjo duniani, GAVI.

Wiki ya chanjo ambayo inaanza leo itaendelea hadi tarehe 30 mwezi huu wa Aprili ambapo pia UNICEF na wadau wanapigia chepuo kampeni kupitia mitandao ya kijamii ya kwamba Chanjo Inafanya kazi, #VaccinesWork.